Zaidi ya vijana 25, 000 wanatarajiwa kushiriki katika Siku ya Vijana Kikanda, itakayoadhimishwa
kuanzia tarehe 7 hadi tarehe 9 Februari 2014, kwenye Jimbo Katoliki la Kaolack, Senegal.
Maadhimisho haya yanapania kuwaonjesha vijana kutoka Barani Afrika uzoefu na mang'amuzi
ya Siku za Vijana Kimataifa. Hiki kitakuwa ni kipindi cha majiundo ya imani, utume
na changamoto ya toba na wongofu wa ndani.
Vijana wanaalikwa kushuhudia furaha
ya kuwa ni Mkristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao pamoja na kukutana na vijana
kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Afrika. Vijana watawashirikisha wenzao furaha
ya kuwa Mkristo na kwamba, kama Jumuiya ya Waamini wanatumwa kwenda sehemu mbali mbali
za dunia kuwaonjesha jirani zao ile Injili ya Furaha na kwamba, Kanisa ni Sakramenti
ya Wokovu hakuna mtu anayebaguliwa!
Akizungumzia kuhusu tukio hili, Askofu
Benjamin Ndiaye wa Jimbo Katoliki Kaolack anabaianisha kwamba, huu ni muda muafaka
kwa Vijana kutoka Barani Afrika kukutana kwa pamoja, ili kutafakari Neno la Mungu
na kusali pamoja. Kardinali Thèodore Adrien Sarr, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dakar,
Senegal atafunga maadhimisho haya kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa hapo
tarehe 9 Februari, kwenye Uwanja wa Michezo wa Lamine Gueye.
Lengo la Ibada
hii ni kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa ajili ya Familia ya Mungu Barani Afrika
inayowalilia watoto wake wanaoendelea kupoteza maisha kutokana na vita, kinzani na
majanga. Ni watoto wa Afrika wanaoteseka kwa kunyanyaswa n akudhuliwa kutokana na
kulazimika kuzikimbia nchi na makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao.
Vijana
watamegewa kuhusu mambo yanayoendelea kulizunguka Bara la Afrika. Ibada hii inapania
pamoja na mambo mengine, kuwatangazia Vijana Barani Afrika Injili ya Kristo; kuwawezesha
vijana kuyafahamu Mafumbo yanayoadhimishwa na Mama Kanisa, ili hatimaye, waweze kuyatolea
ushuhuda wa furaha ya imani, tayari kwenda sehemu mbali mbali za dunia kutangaza Injili
ya Furaha, wakitambua kwamba, wao ni mahujaji wa imani.