2014-02-03 13:52:47

Mfalme Daudi ni mfano bora katika kumpenda Mungu na watu; kutubu na kumwongokea Mungu pasi na kulipiza kisasi!


Mfalme Daudi alikimbia pamoja na watumishi wake kutokana na usaliti uliofanywa na mwanae Absalomu na watu walikuwa wana muunga mkono Absalomu dhidi ya baba yake, jambo ambalo lilimwongezea Mfalme Daudi machungu katika moyo wake.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake siku ya Jumatatu, tarehe 3 Februari 2014, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican anasema, Mfalme Daudi kama kiongozi wa Serikali, alipaswa kufanya maamuzi machungu kwa kutambua kwamba, vita ingekuwa ngumu na watu wengi wangepoteza maisha, anaamua kukimbia ili kuokoa maisha ya watu wake pamoja na mji wa Yerusalemu.

Hapa Mfalme Daudi anaonesha upendo kwa Mungu na watu wake; anatambua udhaifu wake wa kibinadamu na anaanza hija ya toba ya wongofu wa ndani, kwa kutembea huku ameinamisha kichwa chini na bila kuvaa viatu. Dhamiri yake ilimsuta na kumfanya atoe machozi ya uchungu.

Baba Mtakatifu anasema, Mfalme Daudi aliamua kufanya Njia ya Msalaba kama kielelezo cha toba ya ndani, bila ya kujihurumia, anapania kuokoa Sanduku ya Agano pamoja na watu wake kwa njia ya toba. Hiki ni kielelezo cha mdhambi anayetubu na kuanza mchakato wa kukumbatia utakatifu wa maisha.

Mfalme Daudi katika hija yake ya toba ya ndani anakutana na Shimei mwana Gera aliyemrushia mawe na matusi Mfalme Daudi, lakini badala ya kulipiza kisasi, anajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, mwamuzi mwenye haki, atakayemlipia kisasi kwa wakati wake. Anakubali kuona utashi wa Mungu ukitendeka juu yake. Mfalme Daudi ni kielelezo na mfano wa mtu anayepitia giza la maisha na majaribu makubwa, lakini bado anaendelea kubaki mwaminifu kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani.

Ni kiongozi asiyelipiza kisasi, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kutolipiza kisasi. Watu wajenge upendo kwa Mungu na jirani; watubu na kuongoka wanapomkosea Mungu, ili siku moja waweze kustahili kuitwa watakatifu.







All the contents on this site are copyrighted ©.