2014-02-03 09:51:11

Maandalizi ya Juma la Elimu Katoliki nchini Rwanda yazidi kupamba moto!


Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda linaendelea kuwekeza zaidi na zaidi katika sekta ya elimu kwa kutambua kwamba, hii ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaotekelezwa na Mama Kanisa. Maandalizi ya Juma la Elimu Katoliki nchini Rwanda, litakaloadhimishwa mwezi Juni 2014 yanaendelea kwa kasi kubwa. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu "Kwa mfano wa Familia Takatifu ya Nazareth, tujenge shule zetu ili ziwe ni familia".

Tarehe Mosi, Juni 2014, Juma hili litaadhimishwa kwenye Parokia zote nchini Rwanda. Tarehe 14 na tarehe 15 Juni, Maadhimisho haya yatafanyika katika ngazi ya Kijimbo na kilele cha Maadhimisho haya kitaifa ni hapo tarehe 21 Juni 2014 na yatafanyika Kabgayi. Hapa wawakilishi wa wanafunzi, wazazi, walezi, walimu pamoja na wadau mbali mbali kutoka katika taasisi za elimu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Rwanda, watashiriki.

Kanisa nchini Rwanda linapenda kuendeleza majadiliano ya kina na Serikali ya Rwanda katika sekta ya elimu na majiundo makini kwa vijana kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Rwanda. Kanisa linaangalia uwezekano wa kuanzisha Mfuko wa Elimu Kijimbo ili kusaidia mchakato wa maboresho ya sekta ya elimu nchini Rwanda.







All the contents on this site are copyrighted ©.