Wafanyakazi hewa wanavyokomba fedha ya Serikali ya Kenya!
Askofu Joseph Mbatia wa Jimbo Katoliki Nyahururu, nchini Kenya amelaani kitendo cha
baadhi ya wafanyakazi wa serikali nchini Kenya kutokuwa waaminifu kwa kuendelea kuchukua
mishahara ya wafanyakazi hewa. Huu ni uchu wa fedha na mali, kielelezo cha kumong'onyoka
kwa tunu msingi za kimaadili na utu wema pamoja na kukosa uzalendo, hali inayoonesha
jinsi ambavyo baadhi ya wafanyakazi wanashindwa kuwajibika.
Hivi karibuni,
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema kwamba, serikali yake inapoteza wastani wa shilingi
Billioni 1. 8 za Kenya kwa kulipa mishahara ya wafanyakazi hewa Serikalini, tabia
inayochochewa na uchu wa mali na fedha miongoni mwa wananchi wa Kenya. Wafanyakazi
wa Serikali wanachangamotishwa kujisadaka kwa ajili ya kuchangia mchakato wa maboresho
ya maisha ya wananchi wa Kenya katika ujumla wao.
Askofu Joseph Mbatia ameyasema
hayo hivi karibuni alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru
Mungu kwa shule ya Msingi ya Yohane Paulo II kuwa kinara katika mitihani ya darasa
la saba nchini Kenya. Amewataka wazazi kuwashirikisha watoto wao furaha na matumaini
kwa kuwaonesha malezi bora na makini. Wazazi waendelee kuwajibika kikamilifu kwa watoto
na jamii kwa ujumla wake.