2014-02-02 14:01:06

Mwaka 2015 ni Mwaka wa Watawa!


Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Sherehe ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya 18 ya Watawa Duniani, tarehe 2 Februari 2014 amekazia umuhimu wa maisha ya kitawa yanayojipambanua kwa kufuata Mashauri ya Kiinjili.

Leo zimetimia siku 40 tangu Mama Kanisa alipoadhimisha Siku kuu ya Noeli, yaani kuzaliwa kwa Yesu Kristo na wazazi wake wakaenda Hekaluni ili kumweka wakfu kwa Bwana kama ilivyoandikwa katika Sheria. Hiki ni kielelezo cha watu wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, kwa kumfuasa Kristo aliyekuwa: mtii, fukara na msafi kamili.

Sadaka hii inawagusa Wakristo wote, kwani wote wamewekwa wakfu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, changamoto ya kusadaka maisha yao kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo, kwa kujitosa kimaso maso kwa ajili ya familia, kazi, huduma kwa Kanisa na matendo ya huruma kwa jirani. Maisha ya wakfu anasema Baba Mtakatifu, kwa namna ya pekee yanajionesha kwa watawa wanaoishi Mashauri ya Kiinjili kwa kujitoa kikamilifu kwa Mungu na Kanisa lake.

Kwa njia hii, watawa wanatoa ushuhuda wa Injili ya Ufalme wa Mungu; tayari kuwapelekea jirani zao mwanga wa Kristo, mahali ambapo bado watu wanaelemewa na uwepo wa giza, ili kuwaonjesha matumaini wale waliokata tamaa! Watawa ni kielelezo cha uwepo wa Mungu katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu; ni chachu ya kukua na kukomaa kwa Jamii katika mchakato wa ujenzi wa Jamii inayosimikwa katika haki, udugu, unabii pamoja na kuwashirikisha maskini na wote wanaoteseka upendo na huruma ya Mungu.

Maisha ya kitawa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni zawadi ya Watu wa Mungu wanaofanya hija ya maisha ya imani. Ni watu wanaohitajika kwa ajili ya kueneza Injili, Mafundisho ya Kikristo, Upendo kwa Maskini, Sala na tafakari; majiundo makini ya mtu mzima: kiroho na kimwili; majiundo kwa vijana, familia pamoja na kuendelea kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani na familia ya kibinadamu.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake unahitaji ushuhuda wa upendo na huruma ya Mungu, changamoto ni kuendelea kuthamini mang'amuzi ya maisha ya kitawa yanayojionesha katika karama na tasaufi mbali mbali. Ni mwaliko wa kuendelea kusali, ili vijana wengi zaidi waweze kukubali mwaliko kutoka kwa Yesu anayeendelea kuwaita vijana kujisadaka kwa ajili ya Kristo na huduma kwa jirani zao.

Baba Mtakatifu kwa kuzingatia mchango mkubwa unaotolewa na Watawa sehemu mbali mbali za dunia, anatangaza rasmi kwamba, Mwaka 2015 Mama Kanisa ataadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani. Tangu sasa Baba Mtakatifu anapenda kukabidhi nia hii njema chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu; kama wazazi wa Mtoto Yesu, walikuwa ni wa kwanza kujiweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu alikumbusha kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, tarehe 2 Februari linaadhimisha Siku ya Uhai. Anaendelea kuvitia shime vyama vya kitume pamoja na wadau mbali mbali wanaojitoa kimasomaso kulinda na kutetea zawadi ya uhai. Waamini na watu wenye mapenzi mema wanakumbushwa kwamba, kila mtoto ni sura ya Mungu anayependa zawadi ya uhai, familia na jamii.

Baba Mtakatifu anawahamaisha waamini, kila mtu katika wajibu na dhamana yake ajitahidi kupenda na kuhudumia Injili ya Uhai. Aipokee na kuiheshimu; Ailinde na kuitetea tangu pale mtoto anapotungwa tumboni mwa Mama yake! Baba Mtakatifu amempongeza Kardinali Augustino Vallini pamoja na wahamasishaji wa kuenzi Injili ya Uhai kutoka Jimbo kuu la Roma pamoja na wasomi ambao wanaendelea kujadili tema hii ambayo ni nyeti katika Jamii







All the contents on this site are copyrighted ©.