2014-02-02 08:45:24

Kituo cha huduma cha Papa Francisko kuzinduliwa Jimbo kuu la Venezia


Kardinali mteule Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anatarajiwa hapo tarehe 5 Februari 2014 kuzindua kituo cha kuwahudumia maskini kilichojengwa huko Marghera, Venezia kutokana na changamoto iliyotolewa na Patriaki Francesco Moraglia wa Jimbo kuu la Venezia. Tukio hili linatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa Kanisa na Kisiasa kutoka ndani na nje ya Venezia.

Hivi karibuni, Patriaki Moraglia alikuwa amemwelezea Baba Mtakatifu Francisko nia ya Jimbo kuu la Venezia kujenga kituo kwa ajili ya kutoa chakula na malazi kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii na kukipatia jina Francisko kwa heshima ya Baba Mtakatifu anayeguswa na taabu na mahangaiko ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Huu ni mchango wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Venezia, Caritas Venezia kutaka kukabiliana na changamoto ya ongezeko la umaskini wa hali na kipato nchini Italia. Kituo cha Papa Francisko ni matokeo ya ukarabati mkubwa uliofanywa kwenye Shule ya zamani ya Edson, ili kutoa nafasi kwa baadhi ya watu wanaokabiliana na hali ngumu ya kiuchumi kwa sasa.







All the contents on this site are copyrighted ©.