2014-02-02 09:07:07

Kanisa litaendelea kuchangia katika ustawi na maendeleo ya Italia na kwa ajili ya mafao ya wengi!


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limehitimisha mkutano wake ulioanza hapo tarehe 27 hadi tarehe 29 Januari 2014 mjini Roma. Marekebisho ya Katiba ya Baraza la Maaskofu katoliki Italia kama sehemu ya mchakato unaopania kujenga na kuimarisha mshikamano na umoja miongoni mwa Maaskofu katika utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa nchini Italia pamoja na kuzingatia Katiba ni kati ya mambo yaliyochambuliwa kwa kina na mapana wakati wa mkutano huu.

Hayo yameelezwa na Askofu Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Maaskofu wanalipongeza Kanisa nchini Italia kwa kuchangia katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Itali pamoja na kuendelea kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi. Maaskofu wameamua kwamba, Baba Mtakatifu ataendelea kuteuwa Rais wa Baraza la Maaskofu katoliki Italia pamoja na Katibu wake ambaye anapaswa kuwa ni Askofu kwa uhuru kamili, baada ya kupewa majina kadhaa yatakayokuwa yamependekezwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.

Maaskofu wamekazia pia umuhimu wa mikutano ya Maaskofu katika Kanda mbali mbali za Italia, katika kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano, ili sauti ya Maaskofu wengi iweze kusikika. Wamefafanua kwa kina na mapana tume mbali mbali za Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, asili, dhamana na wahusika wake wakuu katika utekelezaji wa mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji nchini Italia.

Baraza la Maaskofu limepitia majibu ya maswali dodoso yaliyotolewa na Sekretariei ya Sinodi za Maaskofu kama sehemu ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayofanyika mjini Vatican mwezi Oktoba, 2014. Majibu yaliyotolewa yanaonesha kwamba, watu wana kiu ya kuona tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinalindwa na kuendelezwa.

Ni matumaini ya waamini wa Kanisa Katoliki nchini Italia kwamba, Mababa wa Sinodi ya Familia wataweza kutafakari kwa kina changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wa Familia na hivyo kuibua mbinu mkakati utakaofanyiwa kazi na Mama Kanisa ili kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu na wala si vinginevyo.

Maaskofu wanasema, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhakikisha kwamba linawekeza zaidi na zaidi katika sekta ya elimu kama ushiriki wa Kanisa katika maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa linatambua kwamba, lina mchango wa pekee katika sekta ya elimu, hii ni sehemu ya mikakati yake ya Uinjilishaji Mpya; kumbe, Kanisa na shule ni chanda na pete. Kanisa Katoliki nchini Italia linataka kuonesha ushuhuda na mchango wake katika sekta ya elimu, kwa kuwashirikisha wanafunzi, wazazi na walimu katika utume huu.

Baraza la Maaskofu Italia, hapo tarehe 10 Mei 2014, litaungana na Baba Mtakatifu Francisko kusimama kidete ili kulinda na kutetea dhamana ya Kanisa katika sekta ya elimu.







All the contents on this site are copyrighted ©.