2014-02-01 12:01:02

Wajengeeni vijana uwezo wa kupambana na makali ya maisha!


Mtakatifu Yohane Bosco alijipambanua kwa kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwajengea vijana uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha kwa njia ya eluimu makini na endelevu. Akawa ni mfano wa Baba na Mlezi mwema kwa watoto waliokuwa wanatangatanga bila ya kuwa na mahitaji msingi ya maisha; akawalisha kwa Neno la Mungu, Mkate wa Uzima pamoja na kuwapatia elimu.

Ili kuendeleza utume wa Kanisa miongoni mwa vijana, Mtakatifu Yohane Bosco akaanzisha Shirika la Wasalesiani wa Mtakatifu Bosco na Shirika la Masista wa Bikira Maria Msaada wa Wakristo.

Ni mtakatifu aliyejitahidi kusoma alama za nyakati na kwa kujibu kero za watu wake kwa kujikita katika Uinjilishaji wa kina uliokuwa unamgusa mtu mzima: kiroho na kimwili, changamoto kwa Shirika la Wasalesiani wa Mtakatifu Bosco kusoma alama za nyakati na kuendeleza utume huu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Hii ni sehemu ya mahubiri iliyotolewa na Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma katika Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Bosco, iliyofanyika Jimbo Katoliki Dodoma, mwishoni mwa Juma. Anasema, Mtakatifu Yohane Bosco alihakikisha kwamba, vijana wanapata malezi makini na endelevu katika maisha yao ya kiroho, kiakili na kimwili; akawajengea uwezo wa kupambana na makali ya maisha kwa njia ya ufundi stadi, hapa akawa ameganga tatizo la ukosefu wa fursa za ajira, changamoto kwa Shirika la Wasalesiani katika sekta ya elimu ili kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa kuwapatia vijana elimu makini inayokwenda na wakati!

Mtakatifu Yohane Bosco alikazia umuhimu wa elimu kwa vijana ili waweze kufahamu ukweli na kuutetea, kazi inayopaswa kuendelezwa na Wasalesiani wa Mtakatifu Bosco kwa kuwapatia vijana ujuzi na maarifa pamoja na Mafundisho ya Kanisa. Kazi ya majiundo kwa vijana inahitaji watu wanyenyekevu wanaoshuhudia kwa maneno na matendo kazi kubwa iliyofanywa na mwanzilishi wa Shirika lao.

Askofu Gervas Nyaisonga amewataka vijana wanaopata elimu na majiundo makini kutoka katika shule na taasisi zinazoendeshwa na Wasalesiani wa Mtakatifu Bosco nchini Tanzania kujenga na kudumisha utamaduni wa kupenda kusoma; kwa kukazia maadili na utu wema; ili kuongeza ujuzi, maarifa na ubunifu mambo msingi katika kupambana na mazingira mbali mbali ya maisha katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Vijana wanaosoma kwenye taasisi za Wasalesiani wa Mtakatifu Yohane Bosco wawe ni mabalozi wema kwa vijana wenzao kwa kushiriki kikamilifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili mchakato wa Uinjilishaji Mpya, sehemu mbali mbali watakakobahatika kwenda na kufanya kazi. Wawe ni watu wanaoongozwa na Neno na Amri za Mungu.

Imetayarishwa na
Rodrick Minja,
Dodoma. Tanzania.







All the contents on this site are copyrighted ©.