Sudan ya Kusini itajengwa katima msingi wa haki, amani, ukweli na upatanisho!
Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini limehitimisha mkutano
wake wa dharura ulioanza hapo tarehe 21 Januari hadi tarehe 31 Januari 2014, kwa kutoa
tamko linalowataka wananchi wa Sudan ya Kusini kusimama kidete kujenga na kudumisha
misingi ya haki, amani na ukweli.
Wanawataka viongozi wa kisiasa wanaohusika
katika mgogoro wa kisiasa uliosababisha vita nchini humo kutekeleza bila mashari mkataba
wa kusitisha vita, uliotiwa sahihi hapo tarehe 24 Januari 2014. Maaskofu wanasema,
falsa ya kutumia mtutu wa bunduki kutafuta suluhu za kisiasa imepitwa na wakatu, umefika
wakati kwa wananchi kujizatiti kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.
Wale waliofanya mauaji dhidi ya jirani zao watubu na kusema ukweli kama sehemu
ya mchakato wa kuponya madonda ya chuki na uhasama kati ya wananchi wa Sudan ya Kusini
na kwamba, matukio haya yasijirudie tena miongoni mwa wananchi wa Sudan kwa ndugu
wamoja kuanza kushambuliana na hatimaye, kusababisha vifo na watu kulazimika kuyakimbia
makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao. Maaskofu wanasema, hawawezi
kunyamaza kwani wameshuhudia mauaji ya kinyama kwa watu wa Sudan ya Kusini na Darfur;
kwenye Milima ya Nuba; Abyei na Blue Nile.
Maaskofu wanasema kuna mambo kadhaa
ambayo yamepelekea machafuko ya kisiasa nchini Sudan ya Kusini; mambo ambayo kimsingi
yanapaswa kushughulikiwa kikamilifu ili kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa. Baadhi
ya mambo haya ni: kinzani ndani ya chama tawala; kilio cha utawala bora; rushwa, ubinafsi
pamoja na upendeleo wa kikabila na kindugu katika kugawana nyadhifa na madaraka mbali
mbali; madonda ya chuki na uhasama ambayo bado hayajapatiwa dawa kamili ili yaponywe!
Maaskofu
Katoliki Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini wanasema, kuna haja ya kuanza mchakato wa
ukweli na upatanisho; ili kuponya madonda ya chuki na utengano; watu waweze kusamaheana
na kuanza kupatana tena, ili hatimaye waweze kuishi kwa amani. Ukweli na upatanisho
ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ikiwa kama Sudan ya Kusini inataka
kuishi katika amani na utulivu kwa sasa na kwa siku za usoni.
Serikali na wadau
mbali mbali waanzishe mchakato wa majadiliano ya kweli, kwa kuwahusisha hata viongozi
wa Kidini kwani mchango wao ni mkubwa. Inasikitisha kuona kwamba, katika majadiliano
ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa kivita huko Sudan ya Kusini, viongozi wa kidini waliwekwa
kando kana kwamba, hawana mchango katika maisha na ustawi wa wananchi wa Sudan ya
Kusini. Serikali haina budi kujikita katika ujenzi wa utawala bora pamoja na kuimarisha
taasisi za kidemokrasia bila kutawaliwa na upendeleo na ukabila, sumu ya maendeleo
ya taifa lolote lile!
Maaskofu wanavitaka vyombo vya habari kusaidia kutangaza
na kueneza ukweli; kujenga na kusimamia haki na upatanisho na kamwe visiwe ni sababu
na chanzo cha kutetea chuki na uhasama kati ya watu. Serikali inapaswa kujipanga katika
kurekebisha muundo wa majeshi ya ulinzi na usalama kwa kutoyahusisha majeshi katika
masuala ya kisiasa. Watoto hawana nafasi katika jeshi, kumbe, kuna haja ya kuzingatia
mafunzo na kanuni maadili kwa vikosi vya ulinzi na usalama. Serikali iendelee kuwekeza
katika sekta ya elimu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wake wote.
Wakimbizi
na wahamiaji wanapaswa kupewa haki zao msingi. Wananchi wa Abyei wanahaki ya kuchagua
mustakabali wa maisha yao kwa siku za usoni na kwamba, Kanisa linaunga mkono kura
ya maoni ili kuonesha mwelekeo wao! Kanisa halitakaa kimya kuona kwamba, baadhi ya
viongozi wake wanaburuzwa na kuzuiwa kutekeleza wajibu wao msingi katika maisha ya
watu wanaowahudumia: kiroho na kimwili. Kanisa litaendelea kuunga mkono juhudi za
upatanisho Sudan ya Kusini pamoja na kusaidia Tuma ya taifa ya uponyaji, amani na
upatanisho.
Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini linasema,
Nchi itajengwa katika msingi wa ukweli na haki na amani; kwa kuthamini na kuheshimu
tofauti zilizopo kama utajiri na wala si kikwazo na chanzo cha vita na kinzani. Wananchi
bado wanahamasishwa kusali kwa ajili ya kuombea: haki, amani na upatanisho wa kweli
Sudan ya Kusini.