2014-02-01 16:12:20

Iweni wajumbe na mashahidi wa upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka!


Kanisa linawashukuru na kuwapongeza waamini walei wanaotoka kifua mbele kwenda sehemu mbali mbali za dunia ili kuwashirikisha jirani zao Injili ya Furaha, bila kusahau majitoleo na utume wao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa kwa ujumla. Ili kuendeleza mchakato huu, kuna haja kwanza kabisa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya Kanisa katika kufikiri na kutenda.

Hija ya maisha ya kiroho kwa kila mwamini ni zawadi kubwa kutoka kwa Roho Mtakatifu; zawadi ambayo kimsingi, ina mwelekeo wa Kikanisa; jambo la msingi ni kuwa wasikivu kwa viongozi wa Makanisa mahalia; kutambua na kuthamini utajiri wa watu wanaowashirikisha Injili ya Furaha pamoja na kuteseka kutokana na mapungufu ya kibinadamu yanayoweza kujitokeza pale inapobidi! Mshikamano na Maaskofu mahali ni jambo ambalo waamini wanapaswa kulifanyia kazi katika hija yao ya maisha ya kiroho!

Haya ni baadhi ya mambo ambayo Baba Mtakatifu amewakumbusha Wajumbe wa Ukatekumeni Mpya, walipokutana na Baba Mtakatifu mjini Vatican, Jumamosi, tarehe Mosi Januari 2014, wakiwa wameandamana na umati mkubwa wa watoto na vijana wanaoshirikishwa Injili ya Furaha katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, umoja na mshikamano ndani ya Kanisa ni jambo la msingi ambalo wakati mwingine linaweza kuwadai kuweka kando baadhi ya mambo yanayohitajika katika hija ya maisha na utume wao! Daima wajisikie kuwa ni sehemu ya Kanisa moja na wala si kinyume chake!

Baba Mtakatifu amewakumbusha wajumbe wa Ukatekumeni Mpya kwamba, daima Roho Mtakatifu anawatangulia kule wanakotaka kwenda na Yesu mwenyewe anatembe pamoja nao hata katika maeneo ambayo yanaonekana kuwa ni mbali katika macho, mawazo na tamaduni za watu mbali mbali.

Huko ndiko mahali ambapo Mwenyezi Mungu anapandikiza mbegu ya Neno lake, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanapokuwa ugenini wanajitahidi kujitamadunisha. Wajitahidi kujifunza na kuthamini lugha ya wale wanaowaonjesha Injili ya Furaha, bila kusahau kujifunza utamaduni, mila na desturi zao njema; kwa kufanya hivi, Injili ya Furaha itagusa na kupenya katika maisha ya watu husika.

Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe waliotumwa kutangaza Injili ya Furaha kuhakikisha kwamba, wanasaidiana kwa hali na mali, hasa kwa kuonesha mshikamano wa pekee na wale wanaonekana kuwa ni wanyonge! Wakumbuke kwamba, hawa ni ndugu na dada zao katika Kristo wanaweza kukumbana na majanga wasiyotarajia katika hija ya maisha na utume wao.

Hapa waoneshe uvumilivu na huruma, kielelezo makini cha ukomavu wa kiimani. Uhuru wa kila mwamini hauna budi kuheshimiwa na kuthaminiwa hata nje ya Ukatekumeni mpya, kama sehemu ya kusikiliza wito na mwaliko kutoka kwa Kristo!

Baba Mtakatifu Francisko anawachangamotisha Wanachama wa Ukatekumeni Mpya, kujitahidi kuwaonjesha wengine Injili ya Furaha kwa kujikita katika mambo msingi, yaani katika Injili ya Kristo. Watekeleze dhamana ya Uinjilishaji kwa upendo, huku wakiwaonjesha jirani zao upendo wa Mungu kwa kuwaambia kwamba, Mungu anampenda mwanadamu jinsi alivyo! Anatambua utakatifu na mapungufu yake ya kibinadamu. Wajitahidi kuwa ni wajumbe na mashahidi wa upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka!







All the contents on this site are copyrighted ©.