Injili ya Furaha na Familia ni mada zinazoendelea kufanyiwa kazi na Maaskofu kwa wakati
huu!
Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, Injili ya Furaha na Maandalizi ya
Sinodi ya Maalum ya Maaskofu kuhusu Familia, itakayoadhimishwa mjini Vatican mwezi
Oktoba 2014 ni kati ya mada zilizofanyiwa kazi na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu
Katoliki Kusini mwa Afrika, katika mkutano wake, ulioanza hapo tarehe 22 hadi tarehe
29 Januari 2014, Jimboni Manzini, nchini Swaziland.
Maaskofu wametafakari kwa
kina na mapana umuhimu na changamoto za Waraka wa Injili ya Furaha kwa Maaskofu mahalia
pamoja na mahusiano na majimbo ambayo wamekabidhiwa kuyaongoza wanapotekeleza dhamana
ya kufundisha, kutakatifuza na kuwaongoza watu wa Mungu.
Baraza la Maaskofu
limepitisha majibu yaliyotolewa na wadau mbali mbali kama sehemu ya Maandalizi ya
Hati ya kutendea kazi. Itakubukwa kwamba, haya ni majibu ya maswali dodoso yaliyotolewa
na Sektretarieti ya Sinodi za Maaskofu kwenda katika Majimbo ya Kanisa Katoliki sehemu
mbali mbali za dunia.
Majimbo yamehamasishwa kuandaa siku moja ambamo wataadhimisha
Siku ya Familia Jimbo, ili kuenzi na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia;
tunu ambazo zinakabiliwa na kinzani nyingi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia bila kusahau ubinafsi na uchoyo; mambo yanayousonga moyo
wa binadamu!
Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika wanajiandaa pia kuja mjini
Vatican kwa ajili ya hija ya kitume inayofanywa na Maaskofu walau kila baada ya miaka
mitano. Hija hii inatarajiwa kufanyika mwishoni mwa Mwezi Aprili, hii itakuwa ni fursa
kwa Maaskofu wengi kutoka Kusini mwa Afrika kukutana na kuzungumza ana kwa ana na
Baba Mtakatifu Francisko.
Maaskofu pia wamezindua kitabu kinachozungumzia
majibu ya kichungaji kutoka kwa Kanisa Katoliki katika kukabiliana na changamoto za
kichungaji kuhusiana na ugonjwa wa Ukimwi. Monsinyo Kevin Randall, Katibu wa Balozi
wa Papa nchini Swaziland katika hotuba yake, amewasihii Maaskofu kuendelea kujikita
katika maisha ya sala na unyofu wa moyo, wakijitahidi kuiga mfano wa Baba Mtakatifu
Francisko kwa kuwaendea wale walioko pembezoni mwa Jamii, ili kuwaonjesha upendo na
huruma ya Mungu.
Maaskofu pia walikuwa wamemwalika Rabbi Warren Goldstein aliyepambanua
mikakati ya majadiliano ya kidini kati ya Kanisa Katoliki na Wayahudi Afrika ya Kusini.
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Kusini mwa Afrika linaandaa Waraka wa Kichungaji
utakaozungumzia kuhusu uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Afrika ya Kusini
sanjari na Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu demorasia ya kweli iliporejeshwa
tena Afrika ya Kusini.