AMECEA kuadhimisha mkutano wake wa 18 nchini Malawi kuanzia tarehe 16 - 26 Julai 2014
Maandalizi ya Mkutano mkuu wa 18 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika
Mashariki na Kati, AMECEA, ni kati ya ajenda kuu zilizofanyiwa kazi na Baraza la Maaskofu
Katoliki Malawi, lililoanza mkutano wake mkuu hapo tarehe 28 hadi tarehe 31 Januari
2014 mjini Lilongwe.
AMECEA inatarajia kufanya mkutano wake mjini Lilongwe
kuanzia tarehe 16 hadi 26 Julai 2014, kwa kuongozwa na kauli mbiu "Uinjilishaji Mpya
kwa njia ya wongofu na ushuhuda wa imani ya Kikristo". Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa
na wajumbe wapatao 300 kutoka katika nchi zinazounda AMECEA. Baraza la Maaskofu Katoliki
Malawi limejadili majibu yaliyotolewa kwenye maswali dodoso kuhusu familia kama sehemu
ya mchakato wa maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya
Familia itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014.
Majibu haya yatatumwa kwenye Sekretarieti ya Sinodi za Maaskofu, tayari kwa
maandalizi ya Hati ya kutendea kazi kama inavyojulikana kwa lugha ya Kilatini "Instrumentum
Laboris". Maaskofu wamepembua hali ya Vyuo vikuu vya Kikatoliki pamoja na Taasisi
za Elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa nchini Malawi; Majiundo ya
Makleri pamoja na ulinzi kwa watoto wadogo. Maaskofu pia wameangalia hali ya kisiasa
nchini Malawi sanjari na Maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini humo tarehe
20 Mei 2014.
Mwishoni, Maaskofu pia wamezungumzia kuhusu hatua mbali mbali
zilizokwishafikiwa na Kanisa Katoliki nchini Malawi katika mchakato wa Majadiliano
ya Kiekumene sanjari na tafsiri ya Misale ya Waamini kwa lugha ya Taifa, "Chichewa".