Wanachama wa Ukatekumeni Mpya kukutana na Papa Francisko mjini Vatican tarehe 1 Februari
2014! Vatican hapatoshi!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe Mosi Februari 2014 anatarajiwa kukutana
na kuzungumza na wanachama wa Jumuiya ya Ukatekumeni Mpya, kama sehemu ya maadhimisho
ya arobaini ya utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa watu wa mataifa.
Baadhi ya wajumbe wa Jumuiya hii watatumwa kwenda kutangaza Injili ya Furaha
barani Ulaya, Amerika na Australia. Jumla ya wanachama 1500 watapata baraka na hatimaye
kutumwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenda sehemu mbali mbali za dunia ili kuwatangazia
watu Injili ya Furaha. Baba Mtakatifu amekwisha wahi kukutana na viongozi wakuu wa
Jumuiya ya Ukatekumeni mpya, lakini Jumamosi, itakuwa ni mara ya kwanza kukutana na
Wanajumuiya hawa wanaoanza hija ya maisha yao ndani ya Chama hiki cha kitume.
Wale
watakaotumwa watapewa Msalaba wa Kimissionari na Baba Mtakatifu Francisko ili kwenda
kutangaza hekima ya Mungu inayofumbatwa juu ya Msalaba. zaidi ya watu elfu kumi wanatarajiwa
kuhudhuria katika mkutano huu na Baba Mtakatifu Francisko.
Chama hiki kinapenda
kuendeleza changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanaowahamasisha
Wakristo kugundua tena ndani mwao ile furaha ya Ubatizo kwa kuitolea ushuhuda pamoja
na kuwamegea pia jirani zao!