2014-01-31 10:31:41

Jumuiya za Kikristo ni chumvi na mwanga wa dunia, zinatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Furaha!


Baraza la Maaskofu Katoliki Austria tarehe 30 Januari 2014 limehitimisha hija ya kitume mjini Vatican kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko katika hali ya urafiki kwa kushirikishana mang'amuzi na vipaumbele katika maisha na utume wa Kanisa nchini Austria.

Katika mazungumzo haya, Baba Mtakatifu aliamua kuwapatia Maaskofu hotuba yake aliyoiandika na baadaye wakaendelea na "michapo" kama kawaida, kama sehemu ya kufahamiana na kujenga umoja na udugu katika Kanisa. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amegusia changamoto ambazo zimelikumba Kanisa nchini Austria na kwamba, ziwe ni kikolezo cha Kanisa kujipanga vyema zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Waamini nchini Austria wanaendelea kuonesha mshikamano na kwamba, sadaka na majitoleo kwa jirani zao yameongezeka maradufu. Kanisa limeendelea kupeta katika utoaji wa huduma makini katika sekta ya elimu na afya, daima kwa kujikita katika mafao ya wengi, jambo ambalo Baba Mtakatifu amewapongeza na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Familia ya Mungu nchini Austria inayoendelea kujitoa bila ya kujibakiza, tayari kutoka kifua mbele kutangaza Injili ya Furaha kwa kuishuhudia kwa njia ya utakatifu wa maisha.

Kanisa linatambua kwamba, watoto wake ni wadhambi, lakini hakuna haja ya kukata tamaa na kushindwa kujibidisha katika mchakato wa kutafuta utakatifu wa maisha, kwa kujitakasa na kujipatanisha na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu; tayari kuongoka na kuanza maisha mapya. Baba Mtakatifu anawahimiza Maaskofu nchini Austria kujielekeza zaidi katika kutoa Sakramenti ya Upatanisho, ili waamini waweze kukutana na Kristo.

Familia za Kikristo ni uwanja makini wa Uinjilishaji Mpya, Jumuiya ya kwanza inayoitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kukazia majiundo endelevu katika elimu na katekesi makini, ili waamini waweze kufikia utimilifu wa maisha yao ya Kikristo. Wanandoa wanapaswa kujiheshimu na kudumisha uaminifu kwa wenzi wao wa ndoa, ili kushinda vishawishi na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha ya ndoa na familia, kiasi cha kutikisa misingi ya maisha ya familia. Ikumbukwe kwamba, ni katika familia watoto wanaweza kurithishwa imani.

Baba Mtakatifu anasema, utandawazi na ubinafsi ni kati ya changamoto zinazoendelea kuzikabilia familia nyingi duniani kiasi kwamba, hata mahusiano kati ya wanandoa na utamaduni wa ndoa kwa ujumla vinawekwa mashakani. Utume wa familia upewe msukumo wa pekee kwa kujenga utamaduni wa familia kukutana, kusali na kushirikishana mang'amuzi ya maisha kwa pamoja ili kujenga na kudumisha umoja; kwa kuganga na kuponya madonda, kwa kuchukuliana mizigo.

Familia ni mahali muafaka pa Uinjilishaji na urithishaji wa imani; hapa ni mahali pa sala, changamoto ya kuwa na maandalizi bora kwa wanandoa pamoja na kuwasindikiza katika maisha na utume wao mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Sakramenti ya ndoa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowawajibisha wanandoa na kwamba, upendo kati ya Bwana na Bibi umetakatifuzwa na Kristo mwenyewe, changamoto ya kukuza na kuendeleza utakatifu wa maisha ya ndoa kwa njia ya uaminifu.

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani na msingi wa maisha ya Kiparokia, mwaliko kwa Maparoko kutambua kwamba, dhamana waliyopewa na Mama Kanisa ya kuongoza ni huduma msingi ya maisha ya kiroho na kwamba, Maparoko wajenge utamaduni wa kushirikiana kwa karibu zaidi na wasaidizi wao na waamini walei katika ujumla wao! Kila mwamini katika hali yake ya maisha anaitwa na kutumwa kutangaza Injili ya Furaha katika medani mbali mbali za maisha ya watu.

Utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu ni dhamana na wajibu wa kila Mkristo unaopaswa kutekelezwa kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo na ushuhuda wa uwepo wa Roho Mtakatifu. Kumbe, kuna haja ya kujenga uhusiano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala na Maisha ya Kisakramenti sanjari na kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Jumuiya za Kikristo zitambue kwamba, ni chumvi na mwanga wa mataifa.

Ratiba inaonesha kwamba, kuanzia tarehe Mosi februari hadi tarehe 8 Februari 2014, Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linafanya hija ya kitume mjini Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.