2014-01-30 07:29:32

Maisha ya kitawa katika huduma ya Uinjilishaji Mpya!


Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Novemba 2013 aliwatangazia kwamba, Mama Kanisa kwa Mwaka 2015 ataadhimisha Mwaka wa Watawa, changamoto na mwaliko wa kuangalia kwa namna ya pekee nafasi ya watawa katika maisha na utume wa Kanisa. Itakuwa ni fursa makini kwa Familia ya Mungu kuhamasisha miito mbali mbali ndani ya Kanisa. RealAudioMP3

Kutokana na changamoto hii, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, kunako Mwaka 2015 litaadhimisha Kongamano la Nne Kimataifa, linaloongozwa na kauli mbiu “Maisha ya Kitawa katika huduma ya Uinjilishaji Mpya”. Kongamano hili linatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 20 hadi tarehe 24 Julai 2015 mjini Bangkok. Lengo ni kuendeleza pia changamoto Uinjilishaji Mpya iliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji iliyofanyika mjini Vatican kunako mwaka 2012.

Maandalizi ya Kongamano tayari yamekwisha anza kwa Idara ya Maisha ya Kitawa, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia kutuma maswali dodoso kwa Mashirika yote ya kitawa na kazi za kitume Barani Asia, kujibu ili kuandaa tema zitakayofanyiwa kazi wakati wa kongamano hilo. Watawa wanaulizwa maana ya Uinjilishaji Mpya katika maisha na utume wa Kanisa mahalia, kwa kuzingatia uzoefu na mang’amuzi ya mtawa binafsi.

Watawa wanahamaishwa kutoa ushuhuda halisi wa jinsi ya kutekeleza dhamana ya Uinjilishaji Mpya katika ulimwengu mamboleo. Wanaulizwa jinsi gani wanavyopambana na biashara haramu ya binadamu inayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu Barani Asia. Kwa namna ya pekee, watawa wanaulizwa ni vikwazo gani wanavyokumbana navyo katika maisha na utume wao wa Uinjilishaji Barani Asia. Kuna mambo mengine ambayo pia yanagusiwa kwenye maswali dodoso, yaani mwelekeo wa Bara la Asia katika utandawazi, mapambano dhidi ya baa la umaskini na njaa; utunzaji bora wa mazingira pamoja na uhuru wa kidini.

Watawa wanaulizwa ni kwa jinsi gani ambavyo Kanisa Barani Asia linaweza kutekeleza utume wake wa kinabii kwa ufanisi na tija zaidi kuliko ilivyo kwa wakati huu kwa kuzingatia uhusiano kati ya Serikali na Kanisa; Jamii na Kanisa; Uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa mengine sanjari na majadiliano ya kidini na waamini wa dini nyingine Barani Asia.

Maswali yote ya dodoso yanatakiwa kuwasilishwa mwishoni mwa Mwezi Februari, 2014, ili kuanza maandalizi ya hati ya kutendea kazi kwa ajili ya Kongamano la Watawa Barani Asia, litakalofanyika kunako mwaka 2015 sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.








All the contents on this site are copyrighted ©.