Padre Raymond Saba, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano
maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, baada ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani,
bado kuna haja kwa waamini kuendelea kuimarisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake
kwa njiaya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu!
Baada ya Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani uliotangazwa, ukazinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa
XVI; ukaadhimishwa kwa nguvu na ari kuu na hatimaye kufungwa na Papa Francisko, Wakristo
wasidhani kwamba, hapa mambo yamekwisha, ndio kwanza waamini wanachangamotishwa na
Mama Kanisa kujifunga kibwebwe ili kuimarisha misingi ya imani inayojikita kwa Kristo
na Kanisa lake.
Umefika wakati kwa Wakristo kushuhudia imani yao kwa njia
ya matendo na kwamba, maisha yao yawe ni mahubiri tosha kabisa kwa watu wanaokutana
nao katika hija ya maisha yao hapa ulimwenguni. Wakristo wanahamasishwa kujifunza
imani yao kwa bidii na juhudi kubwa! Wajitahidi kuifahamu, kuilinda na kuitetea!
Ni
mwaliko wa kuikiri kama inavyofafanunuliwa kwenye Kanuni ya Imani; kuiadhimisha katika
Sakramenti mbali mbali za Kanisa na Liturujia; kuimwilisha kwa kufuata Amri za Mungu
na kanuni maadili pamoja na kuisali. Haya ndiyo mambo makuu yaliyokaziwa wakati wa
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani na kweli yanapaswa kuendelezwa kwa ari na kasi kubwa
zaidi kwani bado kuna changamoto nyingi za uvunjivu wa misingi ya uhuru wa kuabudu
pamoja na uwepo wa misimamo mikali ya kidini inayotishia imani na maisha kwa ujumla.
Waamini wasikubali kupoteza dira na mwelekeo wa imani na maisha yao kwa kukosa
msingi thabiti. Ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu anaendeleza Katekesi
kuhusu Sakramenti za Kanisa ni vyema waamini wakajitahidi kuzifahamu na kushiriki
vyema katika maisha ya Kisakramenti, pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu
na jirani, huu ndio muhtasari mkuu wa Imani kwa Kristo na Kanisa lake.