Kanisa Katoliki nchini Swaziland, linaadhimisha Jubilee ya Miaka 100 ya Uinjilishaji
wa kina, sanjari na kumsimika Askofu Jose Luis Ponce de Leon aliyeteuliwa hivi karibuni
kuwa Askofu wa Jimbo la Manzini, Swaziland. Sherehe hizi ambazo zimefanyika hivi karibuni
zimehudhuriwa na wajumbe wa Shirikisho la Baraza la Maaskofu Kusini mwa Afrika, SACBC
pamoja na viongozi wa Serikali ya Swaziland. Baraza la Maaskofu Kusini mwa Afrika
lilikuwa na mkutano wake wa Mwaka Jimboni Manzini.
Askofu mkuu Bhuti Tlagale,
Rais wa Baraza la Maaskofu Afrika ya Kusini amempongeza Askofu Jose Luis Ponce de
Leon kwa kuteuliwa kwake kuwaongoza watu wa Mungu Jimboni Manzini.
Kazi kubwa
iliyoko mbele yake ni kuhakikisha kwamba, anawatakasa kwa njia ya Sakramenti za Kanisa;
anawafundisha Neno la Mungu na Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na kuwaongoza, daima
akijitahidi kuiga mfano wa Kristo Mchungaji mwema. Atoe kipaumbele cha kwanza kwa
maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii, ili waweze kuonja huruma na upendo
wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani.
Serikali ya Swaziland inayoongozwa
na Mfalme Mswati wa tatu, imelipongeza Kanisa Katoliki nchini humo kwa kujimbanua
kwa huduma makini kwa wananchi wa Swaziland: kiroho na kimwili katika sekta ya elimu,
afya na maendeleo endelevu. Hii imekuwa ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina,
ulioanza kucharuka kunako tarehe 27 Januari 1914, Kanisa la kwanza likajengwa Mbabane,
linayojulikana kama Kanisa la Bikira Maria wa Mateso.
Waamini wa Kanisa Katoliki
nchini Swaziland wanakadiriwa kuwa ni laki sita, sawa na asilimia 5%. Wakristo katika
ujumla wao wanaunda asilimia 40% ya idadi ya wananchi wote wa Swaziland. Wananchi
wanaheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao za kiimani, jambo ambalo linasifiwa
sana na Serikali ya Swaziland.
Shirikisho la Baraza la Maaskofu Kusini mwa
Afrika katika mkutano wake, limejadili kwa kina na mapana mchango uliotolewa na Mzee
Nelson Mandela wa Afrika ya Kusini aliyefariki dunia hivi karibuni katika ustawi na
maendeleo ya wananchi wa Kusini mwa Afrika kwa kukazia zaidi: usawa, umoja na mshikamano
wa kitaifa, demokrasia.
Afrika ya Kusini inakabiliwa na changamoto ya kuendeleza
mchakato huu baada ya kifo cha Mzee Nelson Mandela kwani bado kuna mengi yanapaswa
kufanyika katika maboresho ya demokrasia, uhuru na maendeleo ya wengi.