Tume ya Mawasiliano ya Jamii, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispani, tarehe 5 Februari
2014 itatoa tuzo maalum kwa wanahabari waliotukuka katika utume wao kwenye uringo
wa bahari kwa Mwaka 2013.
Lengo la tuzo hii ya hali ya juu kutolewa na Baraza
la Maaskofu Katoliki Hispania inalenga kutambua mchango unaotolewa na wanahabari katika
medani mbali mbali za maisha, kwa kujipambanua zaidi kwa kusimama kidete kulinda na
kutetea utu na heshima ya binadamu; haki msingi za binadamu sanjari na tunu msingi
za Kiinjili.
Kwa mwaka 2013, tuzo hii anapewa Padre Federico Lombardi, Msemaji
mkuu wa Vatican ambaye pia ni Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican. Itakumbukwa kwamba,
miezi michache iliyopita alikuwa pia ni mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Televisheni cha
Vatican. Huu ni utume unaohitaji mtu kujisadaka ili kutekeleza majukumu yote haya
kwa juhudi, maarifa, bidii na weledi.
Waswahili wanasema, kwa Padre Lombardi,
"hapa upele ulipata mkunaji!". Ni kiongozi asiyependa makuu, lakini mwaminifu na mchakapakazi.
Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania pia litatoa tuzo kwa Kampuni ya "Algencia
101" inayosimamia na kuratibu akaunti ya Baba Mtakatifu Francisko @Pontifex. Kampuni
hii imepewa tuzo huu kwa kucharuka katika matumizi ya teknolojia mpya ya njia za mawasiliano
ya jamii.