2014-01-29 09:45:12

Tafakari ya Neno la Mungu kuhusu changamoto za kifamilia!


Kulingana na Sheria ya Musa, wanaume wote wa Israeli, walipaswa kwenda mbele ya Bwana mara tatu kwa mwaka. Matukio makuu waliyopaswa kushiriki ni Sherehe ya Pasaka, Sherehe ya Pentekoste na Sherehe ya Vibanda (soma Kut 12:24-27; 23:15; Kumb 16:1-17)*. Pahala pa kukutana na Bwana palikuwa pale ambapo Sanduku la Ahadi lilikuwepo, chini ya ulinzi wa makuhani. Mwanzoni Sanduku hili lilizunguka sehemu mbalimbali, mwishowe Mfalme Daudi alilifikisha katika Mlima Sioni, ambapo baadaye Mfalme Selemani alilijengea hekalu, jijini Yerusalemu (2Sam 6; 1Fal 8).

Kila Myahudi aliyekuwa akikaa karibu na jiji la Yerusalemu alipaswa kushiriki katika ibada hizi. Kwa Wayahudi wengine waliokuwa mbali ya Nchi Takatifu, ndoto yao ilikuwa kushiriki japo mara moja katika maisha yao. Hivyo, twaweza kufikiria umati wa watu uliokuwa ukikusanyika jijini humu, katika sikukuu hizi za kidini.

Akina mama walikuwa hawafungwi na sheria hii, lakini wengi wao walikuwa wanakwenda kutokana na uchaji wao. Mfano ni familia ya Elkana, baba yake nabii Samweli, mzee huyu na familia yake yote, yaani wake zake na watoto wake walikuwa na desturi ya kwenda Silo kila mwaka, ambako Sanduku la Agano lilikuwepo. Familia hii ilikwenda huku kuhiji na kutoa sadaka pamoja na waamini wengine (1Fal 1:3).

Watoto wa kiume japokuwa wengine walikuwa wakienda kwenye hija hizi, lakini hakuwakuwa wakilazimika kisheria. Watoto hawa wa kiume, walilazimika tu kwenda baada ya kutimiza mika kumi na tatu. Baadhi ya wazazi walikuwa na desturi ya kuwazoeza watoto wao kushika mapokeo haya mwaka mmoja kabla ya kutimiza umri uliotakiwa, watoto hawa waliitwa “wana wa Sheria.” Licha ya wana hawa wa Sheria, wazazi wengi walikuwa wakiwachukua na kwenda nao hija, hata katika umri mdogo kabisa.

Hivyo, hatuwezi kutia shaka kwamba wazazi wa Yesu walikuwa na desturi ya kwenda nae hija Yerusalemu mara zote ambazo wao wenyewe walikuwa wakienda kushiriki maadhimimisho haya matakatifu. Kwa hakika wasingeweza kudiriki kumwacha Mtoto wao huyu wa thamani kuu machoni pao, nyumbani kwao Nazarethi na wao kwenda Yerusalemu.

Mwinjili Luka ndiye anayetuhabari juu ya tukio hili:

Kila mwaka wazazi wake walikwenda Yerusalemu kwa Sikukuu ya Pasaka. Alipotimiza umri wa miaka kumi na miwili, walikwenda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu. Baada ya siku zile, walirudi kwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu, wazazi wake hawakuwa na habari (2:41-43).

Haya hizi tatu, ni sawa na kitunguu, kila unapotoa ganda moja, unakutana na lingine. Hapa Mwinjili Luka anatufundisha mambo mengini. Tuyadodoe machache kwa faida yetu.

Japokuwa kisheria ilitosha kukaa kwa siku moja tu hekaluni, lakini Familia Takatifu ilikaa kwa juma zima la Sherehe ya Mikate Isiyotiwa Chachu, jijini Yerusalemu, kama tunavyoambiwa “baada ya siku zile...” Baada ya kumaliza shukrani yao, Maria na Yosefu walijiandaa kurudi nyumbani kwao Nazarethi, pamoja na ndugu na majirani zao. Wazazi wanarudi nyumbani, Mtoto amebaki Yerusalemu, bila wao kujua. Sababu ya tukio hili, hatuelezwi na mwandishi, ndio maana kuna wengi waliojaribu kueleza sababu ya tukio hili. Tutaje maelezo yote, kwani kila moja lina utajiri wake.

- Yesu alibaki Yerusalemu, bila wazazi wake kujua, kwa kuwa alitumia uwezo wake wa kiungu kuondoka katikati yao, bila kuonekana. Lakini twaweza kujiuliza, chini ya uangalizi makini ya wazazi haya, ingewezekanaje Mtoto huyu kutoonekana siku nzima bila wazazi wake kugutuka?

- Safari ya wahujaji kurudi makwao, baada ya maadhimisho haya matakatifu ilikuwa na utaratibu wake. Ili kutowachanganya wanawake na wanaume, walikusanyika pekee yao, na kuondoka katika jiji takatifu, kundi la akina mama mbele na akina baba wakifuatia. Safari iliendelea hivyo mchana kutwa, mpaka jioni walipofika katika kituo cha kupumzika kwa siku hiyo. Watoto walikuwa huru, ama kuwa katika kundi la akinamama au akina baba. Hivyo, Maria na Yosefu ulipofika wakati wa kuondoka, kila mmoja alijua kwamba Mtoto Yesu yupo na mwenzake katika kundi lao.

Maria d’Agreda, katika maono yake anasema kwamba Maria na Yosefu walikuwa wamezama katika tafakari ya makuu waliyokwisha kuyaadhimisha katika sadaka ya Pasaka hekaluni. Wazazi hawa walijua kuwa Yesu ndiye sababu, mhanga na lengo ya sadaka kuu iliyokuwa ikitolewa na taifa lao. Wazazi waliendelea kupiga hatua mbele, bila wasiwasi wowote, kwani tukio kama hili kamwe halikuwa limewahi kutokea katika familia yao. Tukio hili lilikuwa la pekee na huru, ambalo Mtoto Yesu hakuwa amewahi kuonesha mfano wala dalili zake.

Tukio hili twaweza kulielewa kuwa lilikuwa na mtazamo wa kiungu, kutokana na matukio mengine yaliyotukia wakati wa utume wake.



Bila matukio haya mawili ni vigumu kuelewa kutoonekana huku kwa Yesu, tukizingatia upendo mkuu, malezi mema na uangalizi makini ambao wazazi wake walikuwa wakimpatia siku zote. Kupotea huku hakukutokana na kosa au uzembe wa wazazi. Lakini yalikuwa mapenzi ya Mungu, ili kutoonekana kwake kuoneshe utukufu wa Baba yake, fadhila ya wazazi wake na maongozi makuu ya majaaliwa ya kiungu.

Maria na akina mama wenzake walianza safari mpaka wakafika mji wa Machmas (unaojulikana leo El Bir). Safari yao ilitawaliwa na nyimbo zenye matamanio ya ujio wa Masiya. Twafahamu fika kuwa wakati wa kwenda hija, kulikuwa na zaburi maalumu, Wimbo wa Kupandia (Zabb 120-134). Bila shaka wakati wa kurudi bado kulikuwa na mwangi wa nyimbo hizi si tu mioyoni mwao, bali pia katika midomo yao.

Katika moyo wa Maria kulikuwa na huzuni kwa kukosekana kwa mtoto wake, ambaye alikuwa ni chemchemi ya furaha yake. Lakini kila alivyopiga hatua mbele alikuwa akijifariji kwamba Mwana wake alikuwa, salama katika uangalizi wa baba yake. Hakunung’unika moyoni kuwa mume wake amependelewa kwa kuwa na Mtoto wao pamoja. Mawazo haya haya yalikuwa yanapita katika akili ya Yosefu.

Jioni ilipokuwa ikikaribia waliweza kuziona kuta za mji wa Machmas ambao ndio ulikuwa kituo chao cha mapumziko ya siku kwa wahujaji waliokuwa wakirejea Galilaya. Wazazi hawa wawili walipokutana, kama radi ukweli ukweli ukawatokea, Yesu hayupo kati yao, hakuwa katika kundi la mbele, wala hakuwa katika kundi la nyuma.

Wazazi hawa wawili waligubikwa na huzuni, isiyo na mfano. Tunatambua hili kwa kinywa cha Mama Maria “... tukikutafuta kwa huzuni...” Huzuni yao haikuweza kufichika, Maria Malkia wa huzuni, ambaye moyo wake ulikuwa ni bahari ya huzuni, anamweleza Mtu wa Huzuni, Yeye aliye Ukweli ambaye alijua kina cha huzuni yao. Moyo wa Yosefu ulijawa na jakamoyo lisiloweza kuelezeka.

Kartagena anauliza: kwa nini wote walikuwa na huzuni? Maria alikuwa na huzuni kwa kuwa alikuwa mama, Yosefu alikuwa na huzuni kwa kuwa alikuwa baba, wote kwa pamoja walihuzunika. Upendo wa Maria ulikuwa ni upendo wa Yosefu. Huzuni na upendo wao kwa Yesu ilikuwa sawa, ilikuwa ni isiyoweza kupimika kwa ukuu wala haikuwa na ukomo. Maria ni huzuni na upendo wote, hali kadhalika Yosefu kwa Yesu.

Upendo na upole wa Yosefu kwa ajili ya Mtoto huyu wa kiungu hatuwezi kuelezea; huzuni yake pia ilikuwa kama ya Maria, ni bahari sisi ambao mioyo yetu ni sawa na kidimbwi haiwezi kuzama katika bahari hiyo. Licha ya hali hii, lakini alikuwa na huzuni ya pekee kwa kuwa alikuwa na jukumu maalumu la kumtunza Yesu, je atatoa maelezo gani kwa kuipoteza hazina hii aali ya Mungu?

- Mwandishi mwingine anatupatia ufafanuzi huu, kutokana na maneno haya“Wakamtafuta kati ya ndugu...” Tunaona hapa kwamba hakukuwepo na utengano kati ya Maria na Yosefu, bali walisafiri pamoja. Katika kusafiri huku, Yesu hakuwa karibu nao, waliridhika kwa kuwa walidhani amejichanganya na watoto wenzake wa ndugu na majirani zao.

Je wazazi walaumiwe, kwani kutomwona mtoto kwa siku nzima na wao wasiwe hata na tashwishwi? La hawastahili lawama, hasa kama tutajivika miwani ya desturi za wakati huo. Kulielewa hili, nitoe mfano kwanza: Leo wazazi wanawapeleka watoto wao shuleni kwa magari au boda boda. Aidha, shule nyingi zina mabasi yao, ya kuwachukua na kuwarudisha wanafunzi wao. Lakini kwa sisi tuliosoma ‘enzi za Mwalimu’ tulikwenda shule wenyewe, tena kwa miguu, na shule zenyewe zilikuwa umbali mrefu.

Desturi za wakati wa Yesu, ni kuwa mtoto aliyefikisha miaka kumi na tatu, alifungwa na sheria zote za Musa na hivyo aliwajibika kwa matendo yake mwenyewe. Ulikuwa ni umri wa kujipatia uhuru kutoka katika utawala wa wazazi, ndio maana wazazi walianza kuwaandaa mwaka mmoja kabla, kwa kulegeza baadhi ya maagizo na uangalizi wao, kama kamba ililegezwa kidogo, hivyo walikuwa na uwanda mpanda zaidi wa uhuru.

Japokuwa jambo hili halikuwa linahitajika kwa Mwana huyu wa kiungu, Yosefu aliona fika kuwa anapaswa kuendana na kawaida ya wazazi wengine, ili isijefichuka siri ambayo wazazi hawa wa Yesu walikuwa wanaihifadhi mioyoni mwao. Lakini twaweza kujiuliza, Maria na Yosefu baada ya purukushani zote za utoto wa Yesu, wangediriki vipi kutembea siku nzima bila Yesu kuwepo katikati yao na wao kuwa na amani, kwani akina Herode kamwe hawaishi duniani?

Kupotea huku kati ya wazazi wake bila shaka lilikuwa ni fumbo toka mwanzo. Mungu ndiye aliyeficha siri ya kutokuwepo kwake kati yao. Kutokuonekana kwa Yesu mbele ya wazazi wake kwa siku tatu, akiwa jijini Yerusalemu, ni kivuli cha siku tatu ambazo Yesu alikuwa kaburini!

Kwa Maria huzuni hii, ilikuwa sawa na aliyoipata alipokuwa chini ya Msalaba. Lakini watakatifu wengi wanaamini huzuni ya siku tatu hizi ilikuwa kubwa zaidi. Maria hakupoteza amani yake ya ndani, na hali hii ni ya kustaajabisha na ilimpatia mastahili makuu. Mungu kwa siku hizi tatu alimwacha katika hali ya neema ya kawaida, alimnyima upendeleo maalumu ambao roho yake ilitajirishwa nao wakati mwingine.

Maria anatuambia kwamba na Yosefu pia alihuzunika vikali. Bila shaka faraja aliyoipata toka kwa Maria ilimtia nguvu kuendelea kumtafuta Yesu. Upendo aliokuwa nao Yosefu kwa Mtoto huyu wa kiungu ulimsukuma kumtafuta bila kupumzika au kula. Baada ya siku tatu za mahangaiko na huzuni, hamadi wanamkuta Mtoto wao hekaluni, katikati ya waalimu “akiwasikiliza na kuwauliza.” Luka anatuambia wale waliokuwa wakimwona na kumsikia, walishangazwa na hekima yake.

Kwa hakika hotuba yake hii ya kwanza, iliwagusa watu, si tu kuwaandaa, lakini kwa baadhi yao, ilikuwa mbegu ya kwanza ya ufuasi. Huyu aliyemfanya Petro katika hotuba yake ya kwanza apate wafuasi lukuki (Mdo 2:41), Yeye mwenyewe kwa hakika hasingeshindwa kupata walau mfuasi mmoja siku hiyo.

Jambo la kustaajabisha hata Maria na Yosefu walishikwa na mshangao “Walipomwona walishangaa...” (2:48). Kulikuwa na kitu kipya kwao, katika sauti yake, jinsi alivyokuwa amekaa mbele ya kadamnasi hii na mtazamo wake. Katika kumbukumbu zao wazazi wao, hawakuwahi kumwona akiwa hivyo. Walipigwa na butwaa, kimya kiliwashika cha furaha na kicho. Yosefu aliendelea kuwa kimya, hakuwa anaamini macho na masikio yake! Kwani kwa nafasi yake ya kiongozi wa familia, alikuwa na haki kumuuliza Mtoto wake nini kilichomfanya habaki Yerusalemu wakati wote walikuwa wanarejea nyumbani, baba huyu hakutoa hata neno moja. Mkewe ndiye anajitokeza mbele na kumuhoji Mtoto wake na Mungu wake “Kwa nini umetufanya hivi...”

Maria hataji kwanza huzuni yake, anataja huzuni ya mume wake kwanza. Twaweza kujiuliza kwa nini anafanya hivi? Mosi, japokuwa mateso ya Maria yalikuwa makuu na yasiyoweza kupimika, hali hii haikumfanya hayasahau machungu ya Yosefu. Pili alifahamu jinsi Yesu alivyompenda Yosefu, ndio maana anataja huzuni ya baba yake kuufanya moyo wa Yesu huguswe na kuona kile alichokitenda kwa yule aliyempenda, kama vile ambavyo Mtoto huyu angekuswa na kutambua jinsi alivyougusa upendo wa mama yake huyu.

Jibu la Yesu “Kwa nini mmenitafuta...” Maana ya jibu hili lenye utata, ilifichika kwa wakati huo kwa wazazi wake, tunaambiwa na mwinjili “Hawakuelewa alilosema.” Kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu na ni Mungu, ya kuwa utume wake hapa duniani ni kuwakomboa wanadamu, kwa njia ya sadaka ya maisha yake mwenyewe, haya yalikuwa wazi kwao, kwani Malaika alishawafunulia hili. Isipokuwa utaratibu, jinsi ya kutelekeza utume wenyewe, eneo na wakati wake, ndio maana katika Arusi ya Kana, Yesu alimwambie mamaye “Saa yangu bado” (Yoh 2:4). Hapa kwa mara ya kwanza twamuona Yesu akifungua pazia na watu wakaweza japo kidogo kuona mwanga wa utukufu wake. Utukufu huu ulonekana vyema mjini Kana, kwa ombi la mama yake (Yoh 2:11).

Tukio hili la Mtoto Yesu kubaki hekaluni peke yake wakati wazazi wake wakirejea nyumbani, ni la kipekee. Mwinjili Luka peke yake ndiye anayetuahadithia tukio hili. Katika masimulizi yake ya utoto wa Yesu, anaanza akiwa Yerusalemu na anahitimisha kwa tukio hili akiwa pia hapo hapo katika jiji takatifu. Yosefu, mtumishi wetu mtukuka naye leo amekamilisha wajibu wake, na kama ilivyo tabia yake anakamilisha wajibu wake katika ukimya, na hatumsikii tena katika masimulizi ya wainjili wetu, bali anabaki nasi katika maombezi yetu, na hasa katika saa ya kifo chetu.

Mtoto aliyekabidhiwa kumtunza, kumlinda na kumlea, ameshafikia umri wa kujitegemea kulingana na Sheria ya Musa, ni mtu mzima, mwenye uhuru katika kutenga na kuwajibika kwa matendo yake. Yukio hili la huzuni, kila Yosefu alipokuwa akilitafakari, lilikuwa ni chemchemi ya faraja.

Moyoni mwake alikuwa anasema, kazi niliyotumwa kuitenda, nimeitimiza, na kama kuna mtu aamini, aende Yerusalemu akawauliza waalimu Sheria!

Tumejifunza nini katika tafakari yetu hii, mintarafu kutoonekana kwa siku tatu kwa Mtoto Yesu, tukio lililowatia simanzi kuu wazazi wake?














Tafakari hii imeandaliwa na Padre Stephano Kaombe
Jimbo kuu la Dar es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.