2014-01-29 07:58:35

Shirika la Masista wa Pendo la huruma wa Mtakatifu Vincent wa Paulo, Mitundu Tanzania


Kuzinduliwa kwa kanda mpya ya Shirika la Masista wa pendo la huruma wa Mtakatifu Vincenti wa Paulo - Mitundu nchini Tanzania ni kielelezo makini cha ushirikiano na ukomavu wa kimissionari, unaowasukuma Wamissionari kutoka sehemu mbali mbali za dunia kujitosa kimasomaso kwa ajili ya ujenzi wa ufalme wa Mungu. RealAudioMP3

Hii ni sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa kazi ya ukombozi wa mtu mzima: kiroho na kimwili. Kunako mwaka 1981 Masista wa kwanza kutoka Innsbruck, Austria waliwasili nchini Tanzania kwa mwaliko wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu waliokuwa wanatekeleza utume wao Jimboni Singida, hususan wilaya ya Manyoni.

Masista hawa wakawa ni wadau wakuu katika azma ya Uinjilishaji kwa kujikita kikamilifu katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu sanjari na katekesi ya kina kwa waamini waliokuwa na kiu ya kufahamu kweli za Kikristo. Wakajenga moyo ya ari ya kulitegemeza Shirika kwa kuwekeza zaidi katika majiundo ya wainjilishaji katika nyanja mbali mbali za maisha. Pengine Shirika la Masista wa pendo la huruma wa Mtakatifu Vincenti wa Paulo ni kati ya Mashirika ya kimissionari yaliyowekeza zaidi katika rasilimali watu na hivyo kuwa na idadi kubwa ya wataalam katika elimu, afya, uchumi na maendeleo endelevu ya Jamii.

Kuundwa kwa Kanda mpya ya Shirika ni matokeo ya uvumilivu na saburi iliyooneshwa na Masista wa kwanza waliowasili kutoka Austria, wakawa tayari kukabiliana na changamoto, vingiti mbali mbali wakati wa ujenzi wa msingi wa Shirika nchini Tanzania pasi na kukata tama. Walijenga na kuimarisha uhusiano wa dhati na wenyeji wa Kata ya Mitundu, kiasi cha kujisikia kuwa wako nyumbani kwani ndani ya Kanisa hakuna mgeni wala mtu wa kuja! Walionja upendo, ukarimu na tunza ya kibaba kutoka kwa Hayati Askofu Bernard Mabula wa Jimbo la Singida, wakasonga mbele kwa ari na matumaini thabiti.

Masita wa pendo la huruma wa Mtakatifu Vincenti wa Paulo - Mitundu, Tanzania, tangu mwanzo walionesha na kujitahidi kujenga mshikamano wa dhati na wananchi wa Kata ya Mitundu, katika raha na shida; mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mafno wa Mungu akapewa kipaumbele cha kwanza katika sera, mikakati na huduma za Shirika. Wakasimama kidete kusikiliza kilio cha wananchi wakati wa baa la njaa, milipuko ya magonjwa pamoja na kuhamasisha elimu kama njia ya kuwakomboa watoto wa wakulima katika baa la umaskini wa hali na kipato. Wakajenga, zahanati na shule na kunako mwaka 1985 huduma za kijamii zikaanza kushika kasi ya ajabu; Kata ya Mitundu ikaanza kucharuka kwa maendeleo ya watu!

Wamissionari kutoka Innsbruck walihitaji mshikamano wa dhati na watawa wazalendo ambao wangeendeleza dhamana na utume waliokuwa wameuanzisha kwa ari na moyo mkuu. Kwa mara ya kwanza msichana Maria Kitiku aliwasili Mitundu, tarehe 19 Machi 1985, huu ukawa ni mwanzo wa hamasa za watawa wazalendo kutoka Tanzania.

Baada ya majiundo ya kina, akafunga nadhiri zake za kwanza kunako mwaka 1989, akawa kweli ni nyota ya matumaini kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii. Wasichana wengi wakavutwa kwa karama na maisha ya Masista hawa, kiasi cha kujiunga nao, leo kuna jumla ya watawa 119 na kuna idadi kubwa ya wasichana walioko kwenye hatua mbali mbali za malezi ya kuwa watawa!

Kuongezeka kwa idadi ya watawa na maboresho ya utume pamoja na kuanza kujitegemea kwa asilimia kubwa, ukawa ni msingi wa kulipandisha Shirika nchini Tanzania ili liweze kuwa n na hadhi ya kituo cha kimissionari, hapo mwaka 1996. Mwaka 2006 wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika wakaamua kwamba, ifikapo mwaka 2012, Shirika nchini Tanzania lijitegemee na kuwa ni Kanda kamili: katika masuala ya uongozi na shughuli za kiuchumi. Mwanzoni watawa wengi walikuwa na wasi wasi ikiwa kama wangeliweza kufanikisha azma hii kwa kujitegemea wenyewe hasa kutokana na changamoto mbali mbali zilizokuwa zinaendelea kujitokeza!

Wakapiga moyo konde na kuanza mchakato wa kipindi cha mpito, wakiongozwa na Padre Gottfried Ugolini kwani walihitaji neema ya kuanza, lakini zaidi neema ya kudumu katika maisha na wito wa kitawa! Kunako Mwaka 2011, Shirika likapata viongozi wa Mkoa wa Tanzania, chini ya uongozi wa Sr. Verediana Herman, aliyesaidiwa na wajumbe wanne. Tarehe 27 Septemba 2013, Masista wa pendo la huruma wa Mtakatifu Vincent – Mitundu- Tanzania, “wakabwaga manyanga” na kutangazwa kuwa Kanda kamili inayojitegemea katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma. Wanashirika wakakabidhiwa Katiba ya Shirika, kama mwongozo na dira ya maisha na utume wao katika mchakato wa kuyamwilisha mashauri ya Kiinjili.

Askofu Msonganzila aliwakumbusha watawa hawa kwamba, Katiba kuu ya Shirika ni Yesu mwenyewe, aliyeteseka, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Yesu anayewashirikisha katika dhamana ya Uinjilishaji, ili watu waweze kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Mwenyezi Mungu. Wanachangamotishwa kuhakikisha kwamba, wanasoma alama za nyakati kwa kumwilisha katiba hii mintarafu mazingira, watu na nyakati. Wakuze ndani mwao ari, wito na utume wa maisha ya Mtakatifu Vincent wa Paulo aliyejitosa kimasomaso bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini.

Masista wa pendo la huruma wa Mtakatifu Vincent- Mitundu- Tanzania wanahimizwa kuwa ni watu wa sala; wakiendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi msingi na endelevu; kwa kujituma kwa juhudi, bidii na maarifa katika kazi, ili kuleta ufanisi na tija katika huduma mbali mbali zinazotolewa na Masista hawa sehemu mbali mbali za Tanzania.

Imeandaliwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.