2014-01-29 08:18:00

Makumbusho ya Vatican ni kati ya vivutio vikuu mjini Vatican, ukibahatika kufika huko nenda kashangae maajabu ya Mungu!


Zaidi ya watu millioni 5. 5 walitembelea Makumbusho ya Vatican katika kipindi cha Mwaka 2013. Hii ni habari njema kwa kuona kwamba, kuna mamillioni ya watu wanaovutwa kutembelea hazina kubwa ya binadamu inayohifadhiwa kwenye Makumbusho ya Vatican. Watu zaidi ya millioni mbili kila mwaka hutembelea kitengo cha “Uffizi”. RealAudioMP3

Mkurugenzi mkuu wa Makumbusho ya Vatican, Bwana Antonio Paolucci anasema kwamba, idadi hii ni kubwa mno kuweza kuhudumiwa kwa ufanisi mkubwa na kwamba, wakati mwingine kuna hatari ya kuweza kuharibu kumbu kumbu hizi kutokana na wingi wa watu pamoja na msongo wa mawazo kwa wahudumu, wanaopania daima kutoa huduma iliyotukuka kwa ufasaha na tija.

Pamoja na changamoto hizi, Makumbusho ya Vatican yanayotembelewa na watu wengi kutoka: Japan, Canada, Chile, Brazil, Australia yataendelea kutoa huduma yake na wala hayana mpango wa kuweka idadi maalum, kwani wengine huwa ni mara yao ya kwanza kushuhudia utajiri huu wanapopata nafasi ya kutembelea mjini Vatican. Wengi wanapenda kushuhudia umahiri wa Sanaa ulioneshwa kwa namna ya pekee kwenye Kikanisa Cha Sistine na kwenye Chumba cha Raphael; Laocòòn na eneo la Apollo Belvedere.

Bwana Antonio Paolucci anasema, uongozi wa Vatican unadhibiti idadi ya watu wanaotembelea Makumbusho ya Vatican kwa kuhakikisha kwamba, kuna mgawanyo mzuri wa watu kwa siku nzima bila ya mwingiliano mkubwa, ili kuwapatia watalii nafasi ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa matendo makubwa aliyomwezesha mwanadamu kuyatenda kwa hekima na busara.

Uongozi unawashauri watalii wanaotaka kutembelea Makumbusho ya Vatican kuhakikisha kwamba, wanafanya mipango yao kwa njia ya mtandao, ili kuokoa rasilimali muda. Mpango huu unaonekana kupata ufanisi mkubwa, kiasi kwamba, Makumbusho ya Vatican yaliweza kupokea watalii zaidi ya millioni 5. 5 katika Kipindi cha Mwaka 2013.

Makumbusho ya Vatican kadiri ya bajeti yake, yataendelea kuboresha Sanaa zilizopo, ili kuleta mvuto zaidi na hatimaye kuzima kiu ya watalii wanaotaka kutembelea utajiri wa Makumbusho ya Vatican. Mkakati huu unakwenda sanjari na ukarabati pamoja na uimarishaji wa hifadhi ya Sanaa zilizopo, kwani penye wengi kuna mengi! Uongozi unajipanga barabara ili kuwa na mapokezi mazuri kwa watalii pamoja na kukabiliana na changamoto mpito kwa kuwapangia vyema watalii bajeti yao!








All the contents on this site are copyrighted ©.