2014-01-29 08:54:34

Jitahidini kuangalia ukweli katika jicho la Kristo!


Katika Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Thoma wa Akwino, Mwalimu wa Kanisa na msimamizi wa Taasisi za Kipapa, Jumanne tarehe 28 Januari 2014, Taasisi za Kipapa zilifanya kikao cha hadhara kilichohudhuriwa na viongozi wa Kanisa, Serikali, Wanadiplomasia na washiriki mbali mbali. Kikao hiki kilikuwa kinaongozwa na kauli mbiu "kuangalia ukweli kwa jicho la Kristo".

Ni maneno yaliyonukuliwa kwenye Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, Mwanga wa Imani, "Lumen Fidei" Waraka ambao kimsingi una uhusiano mkubwa na Waraka wa Injili ya Furaha, "Evangelii Gaudium" ambazo zilifanyiwa tafakari ya kina katika kikao hiki.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa washiriki wa kikao hiki amezungumzia kuhusu nyaraka hizi ambazo ni mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kutafakari mwanga wa imani katika mahusiano kati ya imani na ukweli, kwa kutumia jicho la akili na moyo, yaani kwa kujikita katika upendo, kwani Mtakatifu Paulo anasema watu wanaamini kwa moyo. Ifahamike kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya imani na upendo na kwamba, imani inakuwa na nguvu pale tu inapomwilishwa katika matendo ya huruma na upendo.

Baba Mtakatifu anaendelea kuelezea kwamba, uelewa makini wa imani unabubujika kwa kupokea upendo wa Mungu unaomwezesha mwamini kufanya mabadiliko ya ndani na kumkirimia jicho jipya ili kuona ukweli unaomzunguka. Kabla ya ufufuko Mitume wa Yesu waliutafakari ukweli uliowawezesha kukutana na Kristo mfufuka; wakabahatika kutafakari maisha na mafumbo yake! Hapa Mtakatifu Toma wa Akwino anasema hii ni imani inayoona.

Huu ni mwelekeo makini kwa waamini katika kutenda na mbinu ya kazi kwa wanataalimungu. Inasikitisha kuona kwamba, ukweli kwa nyakati hizi umebaki kuwa ni dhana ya mtu binafsi, kwani ukweli wa wengi unaonekana kuwatisha watu kwani wengi wanautambulisha kuwa ni kielelezo cha utawala mabavu.

Ukweli unapaswa kuwa ni kielelezo cha upendo wa dhati unaotoa fursa kwa watu kukutana na kuendelea kuwa huru kwa ajili ya mafao ya wengi. Mchakato huu unawawezesha waamini kuwa na usalama katika imani pamoja na kuwachangamotisha kuanza hija inayowawezesha kutoa ushuhuda na majadiliano na wote!

Baba Mtakatifu anasema, Mama Kanisa anafanya hija ya kimissionari ili kutangaza Injili ya Furaha, inayopania kumletea mwanadamu mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni changamoto hata kwa Taasisi za Kipapa kufanya mabadiliko ya kweli ili kutoa mchango katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Haya ni mabadiliko yanayogusa mambo msingi, kwa kuzingatia kilicho kizuri, kikubwa, chenye mvuto na ni muhimu. Baba Mtakatifu anazitaka Taasisi za Kipapa kushiriki kikamilifu katika huduma ya utume wa Kanisa zima. Anawatia moyo wanataalimungu vijana kujituma zaidi ili kuleta mwelekeo mpya wa Kikristo. Baba Mtakatifu ametoa tuzo kwa wanasomi vijana wawili: Padre Alessandro Clemenzia na Professa Maria Silvia Vaccarezza waliofanya vyema katika tafiti zao za kitaalimungu.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia kheri na baraka wasomi na watafiti mbali mbali kuendeleza ari na moyo huu, kila mtu katika kitengo chake. Amewaweka wote chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, Kikao cha Hekima. Baba Mtakatifu anaendelea kuwaomba kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala zao!







All the contents on this site are copyrighted ©.