Itawagharimu sana wananchi wa Sudan ya Kusini kuanza ujenzi wa miundo mbinu iliyoharibiwa
kutokana na vita!
Miundo mbinu ya Jimbo Katoliki la Malaka, Sudan ya Kusini imeharibiwa vibaya kutokana
na vita iliyopamba moto kwa takribani mwezi mmoja uliopita. Ujenzi wa miundo mbinu
hii ulifanywa kwa kipindi cha miaka minane ya shida na sadaka kubwa kutoka kwa waamini,
wafadhili na watu wenye mapenzi mema, lakini kufumba na kufumbua kila kitu kimebaki
kuwa ni majivu. Haya ndiyo madhara ya vita inayoshabikiwa na watu wanatafuta madaraka
kwa nguvu bila kuangalia masilahi na mafao ya wengi!
Hayo yamesemwa jumapili
iliyopita, tarehe 26 Januari 2014 na Monsinyo Roko Taban Musa, Msimamizi wa kitume
wa Jimbo Katoliki la Malakal, wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye
Parokia ya Mtakatifu Kizito, Jimbo kuu la Juba.
Maeneo yaliyoharibiwa vibaya
na vita Sudan ya Kusini ni pamoja na Upper Nile, Unità pamoja na Jonglei. Itawagharimu
sana wananchi wa Sudan ya Kusini kuweza kurejesha amani na utulivu kwani hadi sasa
Serikali na Wapinzani wanarushiana "madongo" kwa kuvunja mkataba wa kusitisha vita
uliotiwa sahihi hivi karibuni.