2014-01-29 08:05:31

Baada ya Kanisa Katoliki Austria kukumbwa na mawimbi makali ya bahari, hali sasa ni shwari!


Kardinali Christoph Schonborn, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Austria anasema, Kanisa Katoliki nchini Austria limekumbana na mawimbi mazito yaliyochochewa na baadhi ya waamini ili kuonesha uasi dhidi ya viongozi wa Kanisa, jambo ambalo lilipigiwa debe na vyombo vingi vya habari ndani na nje ya Austria.

Lakini kwa sasa hali ya bahari ni shwari, Kanisa linazidi kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa, kwa waamini kushiriki vyema zaidi katika maisha na utume wa Kanisa, kiasi cha kuanza kuona miito ya maisha ya kitawa na kipadre ikianza kuchipuka na kushamiri kama mtende wa Lebanon!

Bado Kanisa Katoliki nchini Austria linahitaji kujikita katika upatanisho, upendo na huruma, ili kuganga na kuponya madonda yaliyojitokeza kati ya waamini kuhusiana na kile ambacho Wakristo wa Kanisa Katoliki wanaamini na hali halisi ya maisha yao ya Kikristo, kwani hapa kunaonekana kwamba, kuna misigano mikubwa kati ya imani na maisha halisi.

Kanisa bado halina budi kujikita katika majiundo makini na endelevu kwa waamini wake hasa kuhusiana na Neno la Mungu; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na umuhimu wa Sakramenti za Kanisa katika ustawi wa maisha ya kiroho. Maisha ya ndoa na familia ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa, kumbe, kuna haja ya kuangalia hsitoria na watu wakubali kufundwa na historia ili kuboresha hali ya maisha ya ndoa na familia kwa siku za usoni.

Kardinali Christophn Schonborn anasema, kuna idadi kubwa ya watawa wanaotekeleza utume wao nchini Austria, kiasi cha kushirikisha karama na utume wao kwa Familia ya Mungu nchini humo. Huu ndio mwelekeo na changamoto ya kimissionari inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu. Parokia zinapaswa kuwa ni mahali ambapo waamini wanakusanyika ili kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, kwa kutambua kwamba, wao kwa njia ya Ubatizo wanakuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Hapa ni mahali ambako wanapaswa kushiriki kikamilifu katika maishana utume wa Kanisa na kamwe wasijisikie kuwa ni wapita njia au watu wa kuja! Haya ndiyo mabadiliko yanayoendelea kufanyiwa kazi na Baraza la Maaskofu Katoliki Austria. Mkazo kwa sasa ni ujenzi wa Parokia kama Jumuiya za Kikristo ukizingatia idadi ya waamini wa Kanisa Katoliki nchini humo. Kwa njia hii, waamini wataweza kufahamiana na kushirikiana kwa karibu zaidi.

Kanisa pia linaendelea kuboresha uhusiano kati ya Serikali na Kanisa pamoja na kuhimiza maisha ya kisakramenti, lakini kwa namna ya pekee Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inayowapatia waamini nguvu ya kusonga mbele kwa imani na matumaini licha ya magumu wanayoweza kukabiliana nayo katika hija ya maisha yao ya kiroho. Sakramenti ya Upatinisho ni muhimu kwa waamini kutambua ubinadamu wao, ili kuonja upendo na huruma ya Mungu inayojionesha kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.








All the contents on this site are copyrighted ©.