2014-01-28 11:35:50

Mwenyezi Mungu anastahili kupewa sifa na heshima kutokana na ukuu wake!


Waamini wanaendelea kuhamasishwa kumtolea Mwenyezi Mungu masifu ya shukrani na sifa kutokana na ukarimu anaoendelea kuwatendea katika maisha yao kama alivyofanya Mfalme Daudi wakati Sanduku la Agano lilipokuwa linarudishwa mjini Yerusalemu.

Ni mwelekeo kama huu aliouonesha Sara aliposikia habari kwamba, hata katika uzee wake, Mwenyezi Mungu amemwangalia na kumtembelea kiasi kwamba, atabarikiwa kupata mtoto! Jambo hili lilizua kicheko cha furaha kutoka katika sakafu ya moyo wa Sara, mke wa Mzee Ibrahim. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga utamaduni, moyo na ari ya kumshukuru na kumwabudu Mwenyezi Mungu.

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 28 Januari 2014 wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichopo mjini Vatican, sanjari na Kumbu kumbu ya Mtakatifu Toma wa Akwino, Mwalimu wa Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, Sala ya shukrani na maombi si kwa ajili ya vyama vya kitume bali ni mwaliko kwa Wakristo wote, kwani hivi ndivyo anavyostahili kupewa mwenyezi Mungu kutokana na ukuu pamoja na uweza wake.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali kwa moyo wao wote kwani hii haki ambayo anapaswa kutendewa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake!







All the contents on this site are copyrighted ©.