2014-01-28 08:51:26

Masalia ya Mwenyeheri Yohane Paulo II yaibwa mjini Aquila!


Askofu mkuu Giuseppe Petrocchi wa Jimbo kuu la Aquila, Italia amewaandikia waamini wake barua kuonesha masikitiko makubwa baada ya watu wasiojulikana kuvunja Madhabau ya Mtakatifu Petro della Jenca na kuiba masalio ya damu ya Mwenyeheri Yohane Paulo II na kufanya kufuru ndani ya Kanisa, tarehe 27 Januari 2014.

Ni matumaini ya Askofu mkuu Petrocchi kwamba, masalia haya yataweza kurudishwa mara moja, kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya upendo wa Mwenyeheri Yohane Paulo II kwa wananchi wa maeneo ya Aquila. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, vyombo vya ulinzi na usalama vitafanya kazi yake barabara ili wahusika waweze kutiwa nguvuni kwa kusababisha usumbufu mkubwa katika imani ya watu.

Askofu mkuu Petrocchi anawaalika waamini kujibu kashfa hii kwa njia ya sala na upendo kwa kushinda kishawishi cha kulipa kisasi na badala yake waoneshe wema zaidi. Mahangaiko haya wajenge umoja na mshikamano miongoni mwa waamini na Fumbo la Utatu Mtakatifu na kuwa ni kielelezo cha ukombozi.

Kanisa linawaomba walioiba masalia haya kuyarudisha wakati huu Kanisa linapojiandaa kumtangaza Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili kuwa Mtakatifu hapo tarehe 27 Aprili 2014.







All the contents on this site are copyrighted ©.