2014-01-28 11:21:07

Kanisa litaendelea kutangaza Injili ya Furaha, Kujenga na kudumisha mshikamano kati ya watu!


Kanisa linaendelea kuhamasishwa kutangaza Injili ya Furaha kwa watu wa mataifa, kwa kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo; kwa njia ya Tafakari ya Neno la Mungu na maisha ya Kisakramenti; kwa njia sala na matendo ya huruma yanayodhihirisha imani tendaji. Kanisa halina budi kushikamana na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii pamoja na kudumisha moyo na ari ya kimissionari; Mwenyezi Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Maaskofu katoliki Italia, CEI uliofunguliwa rasmi hapo tarehe 27 Januari na unatarajiwa kufungwa tarehe 30 Januari 2014. Maaskofu wanawahimiza waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Italia kujenga na kuimarisha utamaduni wa mshikamano kwa kuondokana na ubinafsi; hali ya kutovumiliana, nyanyaso na mateso kwa watu wasiokuwa na hatia.

Maaskofu Katoliki nchini Italia wanaendelea kukazia umuhimu wa Uinjilishaji Mpya na Kanisa kuendelea kujikita katika sekta ya elimu kwa umma, kama sehemu ya mchakato wa kurithisha imani na tunu msingi za maisha ya kiutu na kijamii. Kanisa linatambua kwamba, huduma ya elimu ni sehemu ya vinasaba na dhamana yake ya Uinjilishaji kwa Watu wa Mataifa. Maaskofu wanapinga kitendo cha shule na taasisi za Kidini kubaguliwa na Serikali katika huduma msingi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linakemea kwa nguvu zote vitendo vya rushwa na ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya wanasiasa kwa ajili ya mafao yao binafsi, kutokana na uchu wa mali na madaraka. Wanawataka wananchi kamwe wasikubali kupokonywa matumaini ya maisha yaliyo bora kwa siku za usoni. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kuwa ni sauti ya wanyonge ndani ya Jamii pamoja na kushirikiana na wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya umaskini na ukosefu wa fursa za ajira kwa vijana.

Kardinali Bagnasco anasema kwamba, Jamii inahitaji wafanyakazi na familia; mambo yanayohitaji ujenzi wa mshikamano wa dhati, kwa kutambua dhamana na utume wa familia ndani ya Jamii. Sinodi Maalum ya Maaskofu kuhusu Familia iliyoitishwa na Baba Mtakatifu Francisko ni kuonesha umuhimu wa familia katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na kutafuta mbinu mkakati wa kichungaji ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika utume na maisha ya kifamilia.

Ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu inapaswa kuungwa mkono katika medani mbali mbali za maisha bila kubaguliwa wala kubezwa!







All the contents on this site are copyrighted ©.