Baraza la Makanisa Ulimwenguni lafanya tafakari ya kina kuhusu ujumbe wa Papa Francisko
kwa ajili ya kuombea amani 2014
Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, hivi karibuni
aliwaongoza wajumbe wajumbe kutoka dini na makanisa mbali mbali kutafakari kuhusu
ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kuombea Amani duniani kwa Mwaka 2014,
uliokuwa unaoongozwa na kauli mbiu “Udugu ni msingi na njia ya Amani”.
Ni ujumbe
unaowachangamotishwa watu wa mataifa kuondokana na chuki, kinzani na uhasama; mambo
yanayoendelea kusababisha maafa na majanga mbali mbali katika maisha ya mwanadamu.
Tafakari
hii iliandaliwa na Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican
kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva pamoja na Jimbo Katoliki la
Lausanne, Geneva na Fribourg. Dr. Tveit anasema, Papa Francisko anawaalika watu wa
mataifa kujenga umoja, udugu na mshikamano, kwa kutambua kwamba, wao kimsingi wanaunda
familia moja ya binadamu. Watu wakishirikiana katika umoja na udugu, haki na Amani
vinaweza kupatikana.
Wajumbe wamempongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa
na kujali mahangaiko ya wananchi wa Syria na Mashariki ya Kati katika ujumla wake.
Dhana ya haki na amani, kamwe haiwezi kuelea katika ombwe, bali ni mchakato unaopaswa
kufanyiwa kazi kila siku ya maisha ya mwanadamu. Ni changamoto kwa Makanisa kuhakikisha
kwamba, yanasimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani katika sehemu
mbali mbali za dunia.