Vijana Wakatoliki Italia wachangia ujenzi wa Kituo cha michezo kwa watoto nchini Haiti
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana aliwasalimia vijana
3000 wa Chama cha Vijana Wakatoliki Italia, waliofanya maandamano makubwa, wakiwa
pamoja na wazazi na walezi wao kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini
Vatican, jumapili iliyopita, tarehe 26 Januari 2014. Haya ni maandamano ya amani yaliyoongozwa
na kauli mbiu "hakuna mchezo bila ya uwepo wako".
Katika ujumbe wao, vijana
hawa wamemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, licha ya mapungufu na karama zao,
bado wanapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, wako tayari kushiriki
katika furaha na upendo wa Mungu wanaonjeshana wakati wanapokuwa michezoni.
Lakini,
si mahali pote kwamba, furaha na upendo huu unaweza kujionesha katika ndiyo maana
katika kujinyima kwao wamekusanya kiasi cha fedha kitakachotumika katika ujenzi wa
kituo cha michezo kwa ajili ya watoto wa Haiti ili kuwajengea tena matumaini na furaha
ya mshikamano wa kidugu.
Watoto hao wawili mvulana na msichana kwa pamoja walirusha
njiwa kama mjumbe wa amani kwa watu wa mataifa, lakini kwa watu wenye kiu ya amani
duniani. Vijana hawa wamemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa unyenyekevu
unaojionesha katika maisha na utume wake.