Ushiriki wa Familia ya Mungu katika maandalizi ya maisha ya ndoa na familia!
Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, kwa mara nyingine tena karibu katika kipindi
chetu cha Kanisa la nyumbani. Baada ya kutazama juu ya maandalizi ya kuingia katika
maisha ya ndoa na juu ya waoanaji wenyewe kuyapa hadhi maisha yao kwa kujiwekea miiko
mbalimbali ya maisha.
Katika kipindi
hiki tuangazie kwa ufupi juu ya ushiriki wa jamii nzima katika kuwasaidia wanandoa
wapya hawa kuanza maisha ya ndoa kwa mwondoko wenye matumaini, utakaowafikisha mbali
katika safari yao ya agano; ambayo ni safari ya kijamii na safari ya kiroho pia; yenye
lengo la kuwafikisha mbinguni.
Miiko ni nidhamu ya maisha. Kuna wakati inauma,
lakini husaidia sana kuzuia hatari mbalimbali ambazo zingeweza kuiyumbisha familia.
Na leo, tujitazame sote kama jamii ya watu ambamo hawa wanandoa wametoka. Tuwasaidieje
ili waanze vizuri, wakue, na wasitawi katika agano lao. Jamii tunaweza kuwasaidia
katika mengi kama vile:- Mosi; TUWAOMBEE! Msaada wa kwanza kabisa au zawadi ya
kwanza ambayo tunaweza kuwapa wanandoa ni SALA. Tuwaweke mikononi mwa Mungu kwa njia
ya sala, ili yule mwovu asiwapepete na kuwamaliza. Hata pale tunapoona “WAMETINDIKIWA
DIVAI”, divai ya upendo, divai ya amani, divai ya maelewano mema, divai ya kuvumiliana,
divai ya uaminifu, divai ya uwajibikaji nk, Ni sisi jamii ya waamini na wanandugu,
ndio tunaopaswa kuchukua nafasi ya Mama wa Yesu katika Arusi ya Kana [Yoh. 2:1-11];
kuwaombea hawa maharusi wetu kwa Bwana tukisema “hawana divai”. Ni kwa msaada wa
sala zetu, tunaweza kuwasaidia hawa ndugu wakaendelea mbele zaidi katika safari yao
ya agano.
Zawadi ya sala, huanza tangu mwanzoni kabisa siku wanapofunga ndoa.
Na hapa, kichungaji tuhimize jambo mmoja; ni vema zaidi watu tukajifunza na tukapenda
kuhudhuria ile ibada au misa ambamo hawa maarusi wanaweka agano lao la ndoa. Tunapokutanika
pamoja mahali pa Ibada, kuinua sala zetu kwa pamoja kwa Mungu ili kuwaombea huruma
na msaada wake, hakika Mungu atasikia kilio chetu. TUNASEMA TENA HILI LITAZAMWE KICHUNGAJI.
Ni
aibu sana nyakati zetu; sehemu inayohusu Ibada kwa Mungu ambapo hawa ndugu zetu wanamwahidia
Mungu kwa kiapo; watu wachache sana wanahudhuria. Ila kwenye ibada za tumbo, yaani
kwenye sherehe, kumbi zinakuwa zimejaa mno. Na hakuna sababu ya msingi ya kutohudhuria
Ibada; NI KUPUUZIA TU, KUTOONA UMUHIMU. Ni wakatoliki walewale, pengine na wana ndugu
pia, hawana msukumo wa kwenda kushiriki IBADA YA NDOA KANISANI; Ila wana muda mwingi
sana wa kushiriki kula tu basi! Eti wanakula michango yao! Hili tulitazame na kulirekebisha
kabla halijawa utamaduni wetu.
Pili, TUWASHAURI: Ushauri ni paji kutoka kwa
Bwana. Sio kila mwenye mdomo anafaa kutoa ushauri. Sio kila mwenye umri mkubwa au
elimu kubwa ana hekima na busara ya kutoa ushauri. Hekima pia ni paji kutoka kwa Bwana.
Endapo UTAOMBWA KUTOA USHAURI, nawe mwenyewe unaona unastahili kufanya hivyo ili kuboresha
maisha ya wanandoa, basi fanya hivyo kwa busara kubwa huku ukiwa na MACHO MAKUBWA
NA KIFUA KIPANA. Yaani, kwa macho makubwa, uwe na ule uwezo wa KUTAZAMA SHIDA HALISI
YA WANANDOA HAWA kwa mapana yake, pasipo kuwa na hila wala upendeleo. Tazama tatizo
ili uwe msaada. Ukiwa na macho madogo, yaani ukiwa mfinyu katika kupembua mambo, utatazama
tatizo na kulitatiza zaidi. Tena uwe na KIFUA KIPANA, yaani UWE NA UWEZO WA KIUTU
UZIMA WA KUTUNZA SIRI. Sio watu wamekushirikisha mambo yao ya ndani kabisa ya ndoa;
wewe unapita kuyaimbaimba mtaani na kumsimulia kila mtu; HAIPENDEZI.
Mpenzi
msikilizaji wa Radio Vatican, kwa leo tunatua nanga, ili nipate nafasi ya kukuandalia
tena ”mabango” kwa makala ijayo, tutakapoendelea kuhekimishana umuhimu wa kuwapatia
wanandoa nafasi, namna ya kutawala na kudhibiti midomo yetu na zaidi ya hayo kutakiana
mema, kwani kuna baadhi ya watu wana roho ya kwanini!
Kutoka Studio za Radio
Vatican ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.