2014-01-27 08:06:22

Jengeni umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana, misimamo mikali ya kidini ni sumu ya maendeleo!


Wananchi wa Nigeria wanapaswa kubadilisha mawazo na mwelekeo wa maisha, ili kujenga na kudumisha upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kuheshimiana, kuvumiliana na kuthaminiana hata katika tofauti zao za kidini na kiimani. Wananchi washikamane zaidi ili kushiriki katika mchakato wa maendeleo ya wengi. RealAudioMP3

Ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Ignatius Kaigama wakati wa Maadhimisho ya Mkutano wa 42 wa Halmashauri Walei Kitaifa. Mkutano huu ulikuwa unaongozwa na kauli mbiu “Nigeria Mpya Inawezekana”. Watu wakionesha uzalendo kwa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi, inawezekana kabisa kuwa Nigeria mpya kwa kuondokana na ubinafsi, uchu wa mali na madaraka. Uzalendo ni jambo la msingi ili kuweza kufikia malengo yanayokusidiwa.

Wananchi wengi wa Nigeria wanamwelekeo wa kujitafuta wenyewe, changamoto ya kubadili mwelekeo utakaogusa maisha ya wananchi wote nchini humo: kuanzia kwa wafanyakazi wa Serikali; Vikosi vya ulinzi na usalama; wanawake na vijana; wasomi na watoto. Kuna haja ya wananchi wa Nigeria kujenga n akudumisha utamaduni wa kuvumiliana kama ilivyokuwa nyakati zilizopita.

Watu waliheshimiana, wakasaidiana, wakaendelea kuishi kwa amani hata katika tofauti zao za kikabila, kiimani na kisiasa. Kimsingi hii ndiyo hali ilivyo sehemu kubwa ya Nigeria, ingawa bado kuna maeneo ambayo wananchi wanaoishi kwa hofu ya kubaguliwa na kushambiliwa. Watu wanadhaniana vibaya kutokana na imani zao za kidini au hata wakati mwingine kuwa na misimamo mikali ya kiimani.

Haya ndiyo yaliyojitokeza kwa Kikosi cha Boko Haram kuanza kuwashambulia Wakristo kutokana na misimamo mikali ya kidini. Mashambulizi haya yamepelekea maafa makubwa kwa wananchi na mali zao. Ni jambo lisilokubalika kwa baadhi ya waamini kutumia jina la Mwenyezi Mungu ili kuwashambulia wengine. Jamii itambue kwamba, kuna baadhi ya watu wanapenda kutumia migogoro ya kidini kwa ajili ya mafao yao binafsi. Hili ni kundi linalopaswa kuogopwa kama “ukoma”.

Wananchi wajenge moyo na ari ya kizalendo, ili kulinda na kutetea tunu msingi za maisha zinazowaunganisha wananchi wa Nigeria katika ujumla wao; kutambua na kuheshimu utofauti unaojitokeza kati yao. Waamini wasimame kidete kutolea ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili na Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Mkutano mkuu wa Halmashauri ya Walei Kitaifa, umehudhuriwa na wajumbe 300 kutoka katika Majimbo 54 yanayounda Kanisa Katoliki Nigeria.








All the contents on this site are copyrighted ©.