2014-01-27 08:26:25

Jengeni na kudumisha utamaduni wa kukutana na watu bila woga, ili kuwaonjesha Injili ya Furaha!


Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, inamwonesha Yesu akianza utume na maisha yake ya hadhara nje ya Mji wa Yerusalem, uliokuwa ni kitovu cha maisha ya kidini, kijamii na kisiasa. Yesu anaamua kuanza utume huu mjini Galilaya ya watu wa Mataifa, mji ambao ulikuwa na watu kutoka katika mataifa, tamaduni na dini mbali mbali, kielelezo cha dunia mamboleo.

Hii ni changamoto ya kujenga na kuimarisha utamduni wa watu kukutana, bila kuwa na woga wala kishawishi cha kutaka kujenga kuta ili kujilinda na kujihakikishia usalama wa maisha. Yesu anawachangamotisha wafuasi wake kutoka kifua mbele ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu, ili kuwaonjesha Injili ya Furaha wale waliokuwa wanaisubiri na hata wale ambao kwa sasa wanaonekana kukata tamaa ya maisha!

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili iliyopita tarehe 26 Januari 2014, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, uliokuwa umefurika kwa umati wa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa kuanzia utume na maisha yake ya hadhara Yesu anapenda kuwafundisha wafuasi wake kwamba, hakuna mtu anayetengwa katika wokovu na kwamba, wote wanashirikishwa na kuonjeshwa huruma ya Mungu.

Hii ndiyo dhamana inayopaswa kuendelezwa na kila Mkristo na Jumuiya zote za Kikristo ili kutoka na kuwaendelea wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; watu wanaohitaji kuona Mwanga wa Injili.

Yesu alianza utume wake nje ya mji na kuwachagua watu wa kawaida kabisa ili kuwashirikisha dhamana na utume wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kati ya wafuasi wake, aliwachagua Mitume na wala hakwenda kwenye shule ya Mafarisayo, Waandishi wala Wanasheria, bali kwa wavuvi waliokuwa wanavua samaki baharini. Hawa wanaitwa na mara moja wanaacha nyavu zao na kuanza kumfuasa Yesu, tangu wakati huo wakajikuta wanaanza maisha mapya!

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, hata leo hii Yesu anaendelea kutembea katika maisha ya kila mmoja wao na kumwita kwa jina ili kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa watu wa Galilaya ya nyakati hizi. Jambo la msingi ni kuwa makini kuisikiliza sauti yake na kufanya maamuzi ya busara kwa kuitikia mara moja ili Injili ya Furaha iweze kuangazia ulimwengu mamboleo.








All the contents on this site are copyrighted ©.