Gharama ya kuunganishiwa umeme kwa wakazi wa Mtwara na Dar imepunguzwa!
Serikali ya Tanzania imeamua kupunguza kwa kiasi kikubwa bei ya kuunganisha umeme
majumbani na kufikia sh. 27,000/ kwa wanavijiji wanaoishi kwenye maeneo ambayo bomba
la gesi linapita. Hatua hiyo imetangazwa Jumapili, Januari 26, 2014, na Waziri wa
Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo wakati akizungumza na wanakijiji wa Mangaka
wilayani Nanyumbu, mkoani Mtwara kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
azindue mradi wa umeme kwenye wilaya hiyo.
“Jana Waziri Mkuu aliagiza tutafute
namna ya kuwasaidia wananchi wanaoishi jirani na njia ya bomba la gesi. Nami nilikaa
na wasaidizi wangu jana usiku na kufanya hesabu na tukaamua tuweke kiwango hicho kwa
ajili ya wakazi hao,” alisema.
Alisema katika mikoa mikoa mingine gharama za
kuunganisha umeme ni sh. 177,000/- lakini kwa mikoa ya Lindi na Mtwara gharama hizo
zilishushwa na kufikia sh.99,000/-. “Lakini sasa hawa wenzetu tumewapa upendeleo zaidi
na tumewapunguzia gharama hizo hadi sh. 27,000/-,” alisema huku akishangiliwa.
Gharama
hizo ni maalum kwa ajili ya wakazi waishio jirani na bomba hilo linaloanzia Mtwara
hadi Dar es Salaam kupitia mikoa ya Lindi na Pwani.
Akizungumza na mamia ya
wakazi wa Mangaka waliofika kushuhudia uzinduzi huo, Waziri Mkuu alisema uzinduzi
wa mradi huo wa umeme ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuhakikisha kila wilaya
inapata umeme.
“Mpango wa kupeleka umeme nchi nzima ni wa miaka mitatu na
katika sekta ya Nishati chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa ya Haraka (BRN), tumeazimia
kwenda kwa awamu ili tuwafikie wananchi wengi zaidi kutoka asilimia 24 ya sasa hadi
kufikia asilimia 30 ya watumiaji wa umeme,” alisema Waziri Mkuu.
Akitoa taarifa
juu ya mradi huo wa umeme wilayani Nanyumbu, Meneja Mwandamizi wa TANESCO, Kanda ya
Dar es Salaam na Pwani inayojumuisha mikoa ya Lindi na Mtwara, Eng. Mahende Mugaya
alisema mradi huo umegharimu sh. bilioni 5.6/- na unatarajiwa kukamilika Aprili, mwaka
huu.
Alisema kuzinduliwa kwa mradi huo kunafanya wilaya zote za mkoa wa Mtwara
ziwe zimepata umeme wa kuanzia na kwamba kazi itaendelea kupitia Wakala wa Umeme Vijijini
(REA) ili kuongeza idadi ya watumiaji wa umeme kwenye mkoa huo.
“Chini ya mfuko
wa REA tumetenga sh. bilioni 7.6 ili zitumike kusambaza umeme katika wilaya zote za
mkoa wa Mtwara ambao sasa hivi watumiaji wa umeme wamefikia 15,675 sawa na asilimia
nne ya wakazi wote wa mkoa huu.”
Alisema katika mwaka 2012-2013 walipata wateja
2,609 tofauti na idadi ya zamani ya wateja 1,300 ambayo ilikuwa imezoeleka. Alisema
hivi sasa wamepokea maombi kutoka kwa wateja 2,588 ambao tayari wamekwishalipia gharama
za kuunganishiwa umeme.
Chini ya mradi wa umeme kupitia REA, jumla ya vijiji
54 katika wilaya za Tandahimba, Masasi na Newala vitanufaika na mradi huo ulioanza
kutekelezwa Desemba 2013 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2015.