2014-01-25 07:37:41

Majadiliano kati ya Kanisa na Serikali ya Ufaransa ni muhimu kwa ajili ya mafao ya wengi!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 24 Januari 2014 amekutana na kuzungumza na Rais Francois Hollande wa Ufaransa na baadaye alikutana na kuzungumza na Kardinali mteule Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na uhusiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo, viongozi hawa wawili wamegusia mchango wa Kanisa katika kutafuta mafao ya wengi nchini Ufaransa; uhusiano kati ya Ufaransa na Vatican pamoja na umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya kina kati ya Kanisa na Serikali, ili kujenga na kudumisha ushirikiano katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ufaransa katika ujumla wao.

Viongozi hao wamejadili pia umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu katika masuala ya: ndoa na familia; maadili katika tafiti; umuhimu wa kuheshimu na kuthamini uhuru wa kidini pamoja na kutoa ulinzi kwa maeneo na nyumba za Ibada.

Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake Rais Hollande katika masuala ya kimataifa wamezungumzia; baa la umaskini, maendeleo na utunzaji bora wa mazingira. Vita na kinzani huko Mashariki ya kati na katika baadhi ya nchi Barani Afrika ni mambo ambayo yamezungumziwa kwa kina na mapana. Viongozi hawa wamekazia umuhimu wa kudumisha msingi wa majadiliano ya kweli kama njia ya kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa pamoja na watu kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao za kidini na kikabila.







All the contents on this site are copyrighted ©.