Wananchi wanaoishi diaspora wanao mchango mkubwa kwa ustawi na maendeleo ya nchi zao!
Dr. James Msekela Balozi wa Tanzania nchini Italia na mwakilishi wa Tanzania kwenye
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko mjini Roma, hivi karibuni ameupongeza Umoja
wa Wanafunzi Wakatoliki Watanzania mjini Roma, kwa kuonesha uhai, umoja, mshikamano
na demokrasia. Ni matumaini ya ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwamba, utaendelea
kuboresha ushirikiano kwa ajili ya mafao na ustawi wa watanzania na Kanisa katika
ujumla wake.
Amesema, umoja
na mshikamano ni mambo muhimu sana katika kukabiliana na hali mbali mbali za maisha,
hasa wanapokuwa ugenini. Amewataka watanzania wanaoishi diaspora kusaidiana kwa hali
na mali pamoja na kufahamiana ili kubadilisha uzoefu na mang’amuzi ya maisha.
Wananchi
wanaoishi “diaspora” wana mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya nchi zao, kumbe,
ni changamoto kwa watanzania kuonesha moyo wa uzalendo na upendo kwa nchi yao kwa
kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maboresho ya maisha ya watanzania wengi.