2014-01-24 08:11:54

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Tatu ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa


Tupo pamoja tena nawe katika jiji la upendo wa Mungu, yaani Neno lake ambalo daima latupatia uzima na pia latufanya tuwe huru katika maisha yetu kama kweli tunaliishi na kulifuata kwa unyenyekevu. Ni Dominika ya III ya kipindi cha kawaida cha mwaka A, kipindi cha matumaini kama ambavyo chajionesha katika mavazi ya Misa Takatifu, yaani rangi ya kijani. RealAudioMP3

Masomo tunayoyatafakari tunayapata katika kitabu cha Isaya 9:1-4, 1Kor. 1:10-13,17 na Injili Mt. 4:12-23. Masomo haya yanatupa mwaliko wa kuona na kuupokea mwanga wa Kristu unaoanza kuangaza kuanzia Galilaya, ndiyo kusema Kristo ni nuru na taa ya kuongoza maisha yetu. Nabii Isaya anatuambia wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu, na wale waliokaa katika uvuli wa mauti nuru imewaangaza. Tena Isaya anaona watu wanavyofurahi, na hivi anatangaza kuvunjiliwa mbali nira ya mizigo ya watu na sasa watu hao wameingia katika uhuru kamili wa wana wa Mungu.

Mpendwa msikilizaji nabii Isaya kama tutambuavyo anaishi katika karne ya 8 kabla ya Kristo. Nabii Isaya anaagua kwa makabila ya Zabuloni na Naftali ambayo yako kasikazini mwa Palestina ambayo hivi leo ni Galilaya. Anapotangaza unabii huu makabila haya yako katika taabu kubwa yaani manyanyaso chini ya Waasiria, ndiyo kusema wako katika giza. Ni katika mantiki hiyo nabii anaona mwanga katika ndoto utakaowafikia watu hawa na kuwaweka huru. Mwanga huu utatokea kwanza pale mlimani Galilaya na polepole utaenea na kuangaza nchi nzima.

Mpendwa msikilizaji, Isaya ataka kusema nini? Anataka kusema kuwa madhulumu yanayowapata ndugu hawa yatamalizwa na mwanga huu ambao utaondoa giza lote, na hivi utawala wa Waasiria utakoma. Kwa hakika mwanga huu ni Kristo Masiha atakayezaliwa na kuanza kuhubiri kuanzia Mlima wa Galilaya. Itachukua miaka 700 hivi, kumbe lazima kutambua kabisa kuwa namna ya utendaji wa Mungu ni tofauti na utendaji wetu. Mungu hutunza ahadi yake hata baada ya miaka mingi kupita.

Tukumbuke ahadi aliyompa Ibrahimu. Hivi leo bado kuna machafuko, vita na mambo kama hayo, je mwanga umekoma kuangaza? Mwanga unaangaza lakini yafaa kufungua macho katika uhuru wangu na kuuelekea mwanga huo vinginevyo hautanifikia na hivi nitaendeleza vita na madhulumu katika ulimwengu huu!

Mpendwa msikilizaji, Mtume Paulo anawakemea Wakorinto ambao wamejenga kuta za migawanyiko na utengano katika jumuiya yao. Ndiyo kusema wengine wanajiona ni wa Paulo na wengine ni wa Apolo na wengine ni wa Kefa na mwishoni wengine ni wa Kristo! Tena mbaya zaidi katika kumega mkate na kunywea kikombe cha divai kila mmoja anafanya peke yake katika kona! Si hayo bali wamejawa na fitina, wivu na kuhukumiana kusikoisha na pia kusikokuwa na miguu wala mikono.

Basi katika haya Mtume Paulo anaanza mafundisho yake akisema Kristo hajagawanyika, ni yuleyule wa jana na leo na daima katika umungu wake. Kwa jinsi hiyo anawaonya na kuwafundisha wakaishi na kupalilia umoja katika jumuiya yao, kwa maana wahubiri wote wa Neno la Mungu yaani Mtakatifu Petro, Apolo na yeye mwenyewe na watakaofuata wanahubiri Neno lilelile ambaye ni Kristu mwenyewe, chimbuko la umoja katika jumuiya.

Anazidi kuwaambia kuwa wahubiri wote ni watumishi katika shamba la Bwana na wala si mabwana katika Kanisa. Mpendwa mwana wa Mungu jambo la utengano liliwapata Wakorinto, je sisi tuko nje ya shida kama hiyo? Kwa hakika jumuiya zetu, familia na mahali pa kazi kuna misukosuko na malumbano na wivu, kumbe yafaa yote kuyasuruhisha tukimtazama Kristu mwanga na chanzo cha maisha yetu.

Katika Injili tunapata kumwona Yesu Kristu katika shughuli za kichungaji huko Kapernaumu, mji ulio pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali yaani katika Galilaya. Kuwa kwake pale ni ili litimie lile neno alilolinena nabii Isaya: Watu wa Zabuloni na Naftali, waliokaa katika giza wameuona mwanga mkuu, mwanga mkuu umewazukia.

Jambo gani anafanya huko ni lile la kutangaza uhuru na ukombozi toka katika uvuli wa mauti. Kauri mbiu ya mahubiri yake huko ni “Tubuni kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia” Mpendwa msikilizaji wakati huohuo akihubiri atawaita na kuwachagua watu kadhaa kwa ajili ya kuingia katika seminari yake wakiandaliwa kwa ajili ya utume wa kuhubiri habari njema.

Tunatambua kuwa Bwana mwenyewe ndiye chanzo cha kila jema ukiwamo wito kwa awaye yote. Wito ni zawadi toka kwa Mungu. Kristu yuko huko kadiri ya injili ya Matayo akianza utume wake hadharani pale katika milima ya Galilaya. Mwanga ule tuliousikia katika somo la kwanza ndo huu sasa unaoanganza kuanzia hapo Galilaya. Ni ukamilifu wa uaguzi wa nabii Isaya. Mpendwa msikilizaji Yesu anachagua kuanzia utume wake hapa Kapernaum, mji mkuu wa Galilaya akiwa na lengo maalumu kadiri ya mwinjili Matayo. Ni lengo gani hio?

Mpendwa, twatambua kuwa watu wa Kapernaum walikuwa ni watu waliodharauliwa na watu wa Yerusalemu, walisadikika kuwa watu wasiokuwa na akili na hata hawakuwa na uwezo wa kufuata sheria, wajinga wa tamaduni zilizofundishwa na marabi. Kwa hakika Kapernaum ilikuwa na mchanganyiko wa makabila tofautitofauti na hii ilikuwa ni sababu mojawapo ya dharau toka kwa Yerusalemu.

Bwana anaanza hapo utume wake hadharani akitaka kusema MWANGA SI TU KWA WALIOWAKAMILIFU BALI HATA KWA WALE WALIOKUWA WAMETENGWA NA JAMII NA HAWA NDIO WA KWANZA KUSHUKIWA NA MWANGA HUO. Mpendwa msikilizaji ili kuupokea mwanga huo ambao ni Kristu lazima kuitikia agizo la Bwana na kadiri ya Matayo ni kutubu na kuamini kwa maana ufalme wa Mungu umekaribia. Toba maana yake ni kubadilisha tabia, mwenendo na kuanza maisha mapya, maisha yanayompendeza Mungu.

Mpendwa msikilizaji, kama tulivyoonesha katika utangulizi sehemu ya II ya Injili inatupeleka kutafakari juu ya wito wa Mitume ndiyo wito wetu hivi leo. Tunaona anawaita mitume 4 wa kwanza, na kwa hakika Matayo hatuambii ni kwa namna gani aliwaita mitume hawa bali anataka kutuambia juu ya wito wetu kama wakristu. Katika kuita Bwana inaonekana anaendelea na utume na safari, akitaka kusema unapoitwa lazima kumfuata kwa haraka na kushughulikia mambo muhimu, si kusimama wala kupumzika na kula na kunywa bali ni hekaheka za kitume katika familia na mahali pote pa kazi.

Mtu anapoitwa kama tunavyoona wito wa hawa ndugu 4 anapaswa kuitika chapuchapu pasipo kuchelewa! Katika kuwaita hawa ndugu wataalikwa kuacha wazazi na kumfuata yeye. Hili laweza kuleta swali mbele yetu! Katika utamaduni wa kiyahudi na hata wa kwetu hivi leo wazazi ndio wanaotuunganisha na mababu na mila za zamani sasa iweje tuachane nao?

Mpendwa msikilizaji ni kweli wazazi wanalojukumu hilo lakini si mila zote zinaendana na Injili, kumbe kuwaacha wazazi kwa Matayo ni kuachana na mila zisizoendana na utamaduni wa MWANGA MPYA UTOKEAO PALE KATIKA MILIMA YA GALILAYA! Mfano wa mila hizo ni kuoa wanawake zaidi ya mmoja, wivu, chuki, ushirikina, uchawi na matunguli yanayozingira maisha na mioyo yetu.

Mpendwa msikilizaji, mitume hawa watakuwa wavuvi wa watu, tofauti na kazi yao ya zamani ya kuvua samaki. Ndiyo kusema watakuwa na wajibu wa kuwaondoa watu katika matatizo mbalimbali ambayo yanawasilishwa kwa sura ya bahari. Kwa hakika bahari katika sehemu hiyo ya Injili yataka kusema, machafuko, nguvu za giza, vita na mambo kama hayo.

Mfuasi wa Kristo kamwe hataogopa kupambana na mizengwe kama hiyo, kwa maana anaongozwa na mwanga tokea Galilaya. Haogopi kuongea na wavuta bangi, watumiao dawa za kulevya na wafanyao mambo kinyume na maadili kulingana na mafundisho ya Kanisa. Mitume ni wale ambao hutenda kazi ya kusaidia wagonjwa kiroho na kimwili wakiwagawia sakramenti za wokovu.

Mpendwa mwana wa Mungu, nikutakie mwitiko daima katika maisha yako ukikumbuka ahadi zako za ubatizo na ahadi nyinginezo katika maisha yako ya Kikristo. Tumsifu Yesu Kristo na Maria Mama wa Mungu.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.