Mzizi wa fitina ya mgogoro wa Urais wakatwa kwa Madagascar kupata Rais mpya!
Rais mteule Henry Rajaonarimampianina wa Madagascar anaapishwa rasmi kuwa Rais wa
Madagascar tarehe 25 Januari, 2014 baada ya Mahakama Maalum ya Uchaguzi nchini Madagascar
kumtangaza Bwana Rajaonarimampianina kuwa mshindi wa uchaguzi wa Urais tarehe 17
Januari, 2014.
Duru ya kwanza ya uchaguzi huo ilifanyika tarehe 31 Julai,
2013, ambapo hakupatikana mshindi. Katika duru ya pili iliyofanyika tarehe 20 Desemba,
2013, Mahakama Maalum ya Uchaguzi ilitangaza kuwa Bwana Rajaonarimampianina alipata
asilimia 53.49 ya kura zote zilizopigwa huku mpinzani wake Bw. Jean Louis Robinson
akipata asilimia 46.51.
Itakumbukwa kwamba, Kwa kushirikiana na wanachama
wengine wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Tanzania, ambayo
ilikuwa mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kwa mwaka mmoja ulioishia
Agosti, 2013, ilitoa mchango mkubwa kuhakikisha Madagascar inaendesha uchaguzi wake
katika hali ya amani na utulivu na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia, ili kumaliza
mgogoro wa kisiasa ulioibuka mwaka 2008 baada ya Bwana Andry Rajoelina kuingia madarakani
kwa kusaidiwa na Jeshi.