Mchango wa Jimbo la Papa katika Mkutano wa Geneva II
Askofu Mkuu Silvano Tomasi, Mwakilishi wa Jimbo la Papa katika Ofisi za Umoja wa Mataifa
za Geneva, kwa niaba ya Jimbo la Papa, ameomba kusitishwa mara moja vita inayoendelea
Syria. Wito huo aliutoa Alhamis katika Mkutano wa Kimataifa wa juu ya mgogoro wa vita
Syria,Mkutano uliopewa jina Geneva II, uliohudhuriwa na wajumbe kutoka maeneo mbalimbali,
hasa nchi za Mashariki ya kati, umoja wa Mataifa na kutoka Shirikisho la Nchi za Kiarabu.
Mazungumzo haya ya amani ya kimataifa, yanalenga katika kujenga amani na maridhiano
yanayoweza kumaliza mgogoro katika Syria.
Askofu Mkuu Silvano M. Tomasi alisema,
vurugu zinapaswa kusitishwa mara moja kwa sababu zimeleta mahangaiko makubwa kwa watu
wa Syria na mkoa huo kwa ujumla . Na kwamba ushiriki wa wanasiasa katika mkutano
a Geneva II, ni ishara ya dhamira ya safi ya kisiasa katika kutoa kipaumbele cha mazungumzano
badala ya utumiaji wa bunduki.Na hivyo , uwakilishi wa madhehebu mbalimbali ya kidini
katika mkutano wao uliotangulia mkutano huu, waliweza kuthibitisha kwa mara nyingine,
njia hii ya mazungumzo kuwa njia pekee na msingi katika kuleta hadhi sawa kwa kila
mtu aliyeumbwa kwa mfano na sura ya Mungu na katika kuwa wazi kwa wengine.
Alielendelea
kusema , wakati umefika wa kuchukua hatua madhubuti, kutekeleza nia nzuri zinazo tolewa
na pande zote katika mgogoro wa sasa. Katika hali hii, Jimbo Takatifu , linarudia
kutoa wito wake kwa pande zote zinazohusika katika mgogoro huu , kukubali kwa moyo
mkunjufu na kwa ajili ya heshima ya utu wa binadamu, kusitisha kila aina ya ukatili
dhidi ya binadamu katika taifa hili pendwa la Syria. Pamoja na wito huo, Jimbo
la Papa limependekeza kusitishwa kwa vita bila ya kuwa na masharti yanayofunga upande
mmoja. Silaha zote ziwekwe chini , na fedha zote zilizolegwa kununua silaha zitumike
katika mipango ya kutoa msaada kwa waathirika wa vita, na huduma nyingine msingi za
kibinadamu. Ukomeshaji wa uhasama lazima uandamane na ongezeko la misaada ya kibinadamu
kama hatua ya kwanza katika ukarabati wa haraka wa maisha ya watu kurudi kawaida.
Vita vimesababisha uchumi wa nchi kuanguka, na hivyo juhudi za kurejesha tena
hali ya kawaida ni lazima kuanza upya kwa pamoja kupitia mazungumzo endelevu na mshikamano
wa ukarimu wa jumuiya ya kimataifa, na katika moyo na mwelekeo wa kidini .
Jimbo la Papa limeonyesha imani yake kwamba, amani Syria inaweza kuwa kichocheo cha
amani katika maeneo mengine ya kanda hii ya nchi za Kiarabu.
Askofu Mkuu Tomasi,
alihitimisha mchango wa Jimbo la Papa, na maneno ya Papa Francisko, yaliyozitaka
pande zote katika mgogoro huu kusikiliza dhamiri yao kwa kina na kutojifungia katika
nia zao binafsi , bali kutenda kwa manufaa ya wote kama ndugu na kwa ujasiri kuamua
kufuata njia ya kukutana na majadiliano, na hivyo kuondokana na upofu unaoleta migogoro.
Papa alihimiza wakumbuke si utamaduni wa mapambano wala utamaduni wa migogoro unaoweza
kujenga maelewano ndani na baina ya watu, lakini badala yake ni utamaduni wa kukutana
na utamaduni wa mazungumzo , ndiyo njia pekee ya kufikia amani endelevu.