2014-01-24 07:54:20

Mchakato wa kushirikishana imani Amerika ya Kusini


Kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani tarehe 25 na tarehe 26 Januari 2014, zitakuwa ni siku maalum kwa ajili ya kukusanya mchango kwa ajili ya kuyasaidia Makanisa yaliyoko Amerika ya Kusini katika maisha na utume wake. RealAudioMP3

Kampeni ya Mwaka 2014 inaongozwa na kauli mbiu ”Kushirikishana Imani”. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, linatambua na kuthamini mchango na zawadi kubwa ya imani kutoka kwa waamini wa Makanisa ya Amerika ya Kusini.

Ni mwaliko na changamoto ya kuhakikisha kwamba, wanaendelea kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, tayari kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoibuliwa katika maisha ya kiroho na kiimani. Wajitahidi kusimama kidete kulinda na kutetea imani yao kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linaendelea kusema kwamba, licha ya kuyapatia msaada wa hali na mali, Makanisa ya Amerika ya Kusini, lakini Wamerikani wanayo mengi ya kujifunza kutoka kwa Waamini wanaoishi huko Amerika ya Kusini.

Mchango wa hali na mali kwa ajili ya Makanisa ya Amerika ya Kusini ulianzishwa kunako mwaka 1965, mara tu baada ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, tangu wakati huo, imegota miaka 50 ya upendo na mshikamano kwa Waamini wa Makanisa ya Amerika ya Kusini. Mchango huu unapania pamoja na mambo mengine kusaidia mwendelezo wa huduma za kichungaji zinazotolewa katika nchi 25 zilizoko Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbiani.

Kipaumbele cha kwanza kinatolewa kwa miradi ya Uinjilishaji na Katekesi, kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa Uinjilishaji Amerika ya Kusini. Hii ni changamoto iliyotolewa na Maaskofu wa Amerika ya Kusini katika mkutano wao maalum uliofanyika kunako Mwaka 2007 huko Aparecida. Waamini wote wanaalikwa na kuhimizwa kuwa ni mashahidi na wamissionari kwa kutangaza Injili ya Furaha katika medani mbali mbali za maisha.

Waamini watambue kwamba, kwa kutekeleza wajibu na dhamana hii, wanashiriki kikamilifu katika utume wa Kanisa la Kiulimwengu, linalotumwa kutangaza Injili hadi miisho ya dunia. Kwa miaka ya hivi karibuni, kiasi kikubwa cha mchango uliotolewa, kilipelekwa kusaidia ujenzi wa Haiti mpya baada ya kukumbwa na tetemeko la ardhi kunako mwaka 2010 na hivyo kusababisha maafa makubwa.








All the contents on this site are copyrighted ©.