2014-01-24 14:57:35

Mawasiliano lazima yaendeleze utamaduni wa kukutana


Alhamis, mjini Vatican, uliwasilishwa Ujumbe wa Papa Francisko kwa ajili ya adhimisho la 48 la Siku ya Mawasiliano Duniani, ambayo itakuwa tarehe Mosi June 2014. Ujumbe wa Papa uko chini ya Mada, “ Mawasiliano katika huduma ya Utamaduni wa Kweli wa Kukutana”.Na ulitolewa Alhamis kama sehemu ya kumbukumbu ya Maadhimisho ya Siku Kuu ya Msimamizi wa Vyombo vya habari na wanahabari, Mtakatifu Francis de Sales, ambayo huadhimishwa tarehe 24 Januari kila mwaka. .
Papa Francisko katika ujumbe huu , anasisitiza kwamba, si vyema kuwasilisha Injili kwa wengine iwapo sisi wenyewe mioyo yetu haiko wazi katika maisha ya Kiinjili na katika kusikiliza ukweli wa wengine. Ujumbe huo unasisitiza kwamba, kuwa shahidi wa kweli wa Kristu si uhodari wa kuwajaza watu na maneno mengi ya kidini lakini hasa ni kujaribu kujibu maswali na mashaka yao, kwa heshima na unyenyekevu katika maisha ya kiinjili.
Askofu Mkuu Claudio Celli , Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mawasiliano ya Jamii, akiwasilisha ujumbe huo kwa wanahabari, alitoa muhtasari kwamba, unjumbe wa Papa, una vipengere mbalimbali vinavyogusa maisha ya kijamii kwa wakati huu , kuanzia utandawazi katika mawasiliano. Unasisitiza vyombo vya habari na teknolojia ya mawasiliano ya kisasa, vitusaidie kutukutanisha kwa ukaribu zaidi na kushirikishana mawazo kwa haraka hata na watu wanaoishi katika maeneo ya ndani vijijini kusiko fikika kirahisi.
Na kwamba utamaduni wa kukutana unadai si tu kuwa watu wa kutoa lakini pia kupokea. Na pia mfumo wa utandawazi,uweze kuhamasisha watu kukutana na kushirikishana na kujenga mshikamano. Papa ameeleza kwa kutazama uwepo wa kashfa ya pengo kati ya utajiri wa matajiri na umaskini mkubwa wa maskini, akionyesha tumaini lake kwamba, vyombo vya habari vinaweza kusaidia kutoa kwa nguvu zaidi maana ya umoja wa familia ya kibinadamu .

Aidha Papa Francisko, akiutazama upande wa pili wa mfumo huu wa mawasiliano ya haraka, ameonyesha kutambua na kukubaliana kwamba kuna changamoto nyingi na halisi , kwa kuwa pia unaweza kujenga utengano na uhasama kati ya watu kwa haraka sana. Lakini hili halihalalishi kupinga maendeleo ya njia za mawasiliano, ila inakumbushwa kwamba, utalaam huu katika mawasiliano si hatima ya binadamu lakini ni mafanikio tu katika teknolojia. Na hivyo Kanisani lazima, liwe mfano katika matumizi mazuri ya nishati hii .
Papa pia ametumia mfano wa msamaria mwema, katika kuona umuhimu wa kuwa tayari kusaidia wengine, utayari wa kuchukua jukumu la kubeba shida na mateso ya wengine. Na kwamba, katika mapinduzi haya ya vyombo vya upashanaji habari na teknolojia ya habari, changamoto kubwa za kusisimua, tunaweza kukabiliana nazo kwa nguvu mpya na mawazo mpya kwa njia ya kushirikishana habari za uzuri wa Mungu na watu wengine.










All the contents on this site are copyrighted ©.