Wivu , chuki, kijicho na uzushi huleta mgawanyiko unaoharibu umoja wa Wakristu.
Mapema Alhamis hii, ikiwa ni siku ya Sita katika Wiki Maalum ya Kuombea Umoja wa Wakristu,
Baba Mtakatifu Fransicko akiongoza Ibada ya Misa katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta
ndani ya Vatican, ameonya kwamba, wivu, chuki na hasida, huleta migwanyiko na utengano
unaoua umoja wa Wakristu. Papa alieleza kwa kutafakari masomo ya Siku ambamo somo
la kwanza, linazungumzia ushindi wa Israeli dhidi ya Wafilisti kupitia ujasiri wa
kijana mdogo Daudi. Furaha ya ushindi wa Daudi, mara inayogeuka kuwa huzuni, wivu
na chukizo kwa Mfalme Saulo, mbele ya wanawake waliokuwa wakimsifu Daudi kwa kumuua
Goliati. Hivyo, ushindi mkubwa wa Daudi unakuwa sababu ya Mfalme Saulo, kujenga
chuki dhidi ya Daudi , kama ilivyotokea pia kwa KainI, ambaye moyo wake uliliwa na
mdudu wa husuda na wivu dhidi ya mafaniko ya ndugu yake Abel. Na ndivyo wivu na husuda
unavyorarua pia mioyo yetu , kwa kutujaza chuki na uovu wa kutovumilia wengine, ndugu
zetu wake kwa waume, wanaopata mafanikio ambayo sisi hatuna. Papa Francisko anasema,
Wivu huongoza katika mauaji. Wivu ni mlango mkuu alioingilia shetani duniani , kama
Biblia inavyosema : kwa wivu wa shetani, maovu yaliingia duniani. Wivu na chuki hufungua
milango yote ya mambo maovu, ikiwepo migawanyiko ya kijamii. Hata Jumuiya ya Kikristo,
huweza kumwezwa na dhambi hii ya wivu na chuki na ubinafsi, unaoelekeza katika kujitenga
na wengine. Papa ameiitia kuwa hii ni sumu kali, kama tunavyoona katika habari za
Kain na Abel. Papa aliendelea kumweleza mtu mwenye wivu, kuwa si mtu wa amani,
ni mtu mkali asiyejua kusifu, wala maana ya furaha.Daima ni mtu wenye kutazama wengine
kwa kijicho na fitina kwa nini yule anavyo na nini mimi sina. Na hii husababisha
uchungu, , uchungu mkubwa unaoweza kuenezwa kwa jamii nzima. Wivu ni silaha ya shetani
katika kuharibu wengine. Papa ameeleza na kurejea Injili ya Yohane inayosema, "kila
anayemchukia ndugu yake ni muuaji". Na alimalizia homilia yake akisema , leo hii,
na tutoleee maombi yetu kwa Bwana kwa ajili ya Jumuiya zetu za Kikristo , ili ziweze
kuiong’oa mbegu hii ya wivu na kamwe isipandwe kati yetu , maana wivu hauna nafasi
katika mioyo yetu, na katika moyo wa jumuiya zetu,. Ila tuweze kusonga mbele na
sifa kwa Bwana. Na kumsifu Bwana kwa furaha, ni neema kubwa , neema ya kutoanguka
katika huzuni na wasiwasi na upinzani unaozushwa na wivu, husuda na kijicho.