Wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Roma wapongezwa kwa umoja, mshikamano na udugu
Mama Josephine Gaita, Balozi wa Kenya nchini Italia ni kati ya wageni mashuhuri waliohudhuria
Ibada ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, wakati Mafrateri wa Shirika la Upendo, maarufu
kama Rosmini walipokuwa wanapewa Daraja ya Ushemasi mjini Roma, hivi karibuni. Mashemasi
hao wapya ni: Fulgence Oisso Epimaki kutoka Tanzania na Shemasi Richard Mwanzia Munyao
kutoka Kenya.
Balozi Gaita ambaye yuko nchini Italia kwa kipindi cha miaka
mitatu sasa amewapongeza wananchi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuonesha
umoja, mshikamano na upendo wa kidugu wakati wa Ibada ya Misa Takatifu. Anasema, alishangazwa
kuona umati mkubwa wa Mapadre, Watawa na Waamini walei walioshiriki katika Ibada hii
kutoka Afrika Mashariki.
Balozi Gaita amewataka Mashemasi wapya kuwa waaminifu
kwa wito na maisha waliojichagulia wenyewe, tayari kumtumikia Mungu na jirani zao
bila ya kujibakiza. Kamwe wasikate tamaa kwani kuna Familia ya Mungu kutoka Afrika
Mashariki inayowasindikiza katika maisha na utume wao kama Makleri.