2014-01-23 07:51:25

Utume wa Vijana Nchini Angola


Baraza la Maaskofu Katoliki Angola katika mkutano wake wa kumi na tisa, limetafakari kwa kina na mapana mbinu na mikakati mipya ya kutangaza Injili ya Furaha kwa watu wanaoihi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kwa namna ya pekee, Baraza la Maaskofu linapenda kuwekeza zaidi katika malezi na majiundo ya vijana nchini Angola. RealAudioMP3

Baraza la Maaskofu Katoliki Angola linasema, kuna haja ya kuwa na mikakati endelevu kwa ajili ya malezi na majiundo makini kwa vijana, kwa kuibua mbinu mkakati utakaoliwezesha Kanisa kusimama kidete kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa kizazi hiki.

Maaskofu wanasema, Kanisa linakabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wake, lakini Uinjilishaji Mpya, uwe ni nyenzo makini ya kukabiliana fika na changamoto hizi, zinazoendelea kutikisa misingi ya imani, utu wema na maadili. Kuna mambo mengi ambayo kwa sasa kwa kisingizio cha uhuru, utandawazi na maendeleo ya sayansi yanasigana kabisa na tunu msingi za Injili na utu wema.

Baraza la Maaskofu Katoliki Angola linasema kwamba, vijana wanapaswa kuwa ni wadau wakuu katika azma ya Uinjilishaji Mpya kwa kuwajengea uwezo ili kuwashirikisha zaidi na zaidi katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu wanakumbusha kwamba, kimsingi dhamana na wajibu wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu ni kwa Wakristo wote. Umefika wakati kwa vijana wa Angola kutoka kifua mbele kutangaza Injili ya Furaha kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na utu wema.








All the contents on this site are copyrighted ©.