2014-01-23 07:42:29

Madhara ya utumwa mamboleo katika maisha na utu wa mwanadamu!


Utumwa mamboleo ni biashara inayoendelea kukua na kushamiri kwa kasi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. RealAudioMP3

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu million 30 wanaoathirika kutokana na utumwa mamboleo na kwamba, biashara hii chafu inawaingizia wahusika kiasi cha dolla za Kimarekani billion moja kwa mwaka.

Utumwa mamboleo ni mtandao mkubwa unaojikita katika soko la kimataifa linalojihusisha na bidhaa za: chakula, mavazi na vifaa vya umeme. Kimsingi hizi ni bidhaa zinazotumiwa na watu kila siku ya maisha yao, huko ndiko wajanja walikotega mitego yao ya kifisadi. Hii ni changamoto kwa watu mbali mbali kuangalia kwa makini matumizi ya bidhaa na huduma wanazonunua sokoni kwani kuna baadhi ya bidhaa hizi zinatengenezwa na watu wanaonyanyasika utu na heshima yao kama binadamu.

Huu ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Silvano Maria Tommasi, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss, kuhusu biashara ya utumwa mamboleo. Anasema, kuna aina nyingi za utumwa mamboleo ambazo zinaendelea kujitokeza katika Jumuiya ya Kimataifa na kwamba, kuna haja kwa Jamii kusimama kidete kupigana kufa na kupona dhidi ya biashara hii inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu, kwa kumgeuza mwanadamu kuwa kama bidhaa nyingine yoyote inayoweza kuuzwa na kununuliwa sokoni. Biashara hii inawatajirisha baadhi ya watu ndani ya Jamii.

Ni biashara inayowatumbukiza watoto katika kazi za suluba zinazotekelezwa katika mazingira hatarishi. Kuna kundi kubwa na wanawake na wasichana wanaotumbukizwa katika biashara ya ngono na kazi za nyumbani kwa ujira “kiduchu”. Kuna wavulana na wasichana wanaolazimika kufanya kazi chafu kinyume cha utashi wao na wala hawana haki ya kuomba ujira sahihi. Watu wanaotumbukizwa katika utumwa mamboleo ni matokeo ya biashara haramu ya binadamu na vitendo vya uhalifu na uvunjaji wa sheria, maadili na utu wema.

Hili ni “janga” linalofahamika na Jumuiya ya Kimataifa, lakini bado hakuna utashi wa kisiasa na kisheria kutaka kudhibiti mchezo huu mchafu. Kuna makundi makubwa ya watu yanaendelea kuzama na kufa maji baharini; wengine wanapotea na kufa kwa njaa na utupu Jangwani Sinai, wakijaribu kutafuta uhuru, ubora na unafuu wa maisha. Haya ni matokeo ya utamaduni unaofumbatwa katika uchoyo na ubinafsi usiozingatia na kuheshimu utu na heshima ya binadamu; tunu msingi za kiutu na kimaadili ambazo zimejisimika katika maisha ya mwanadamu.

Askofu mkuu Silvano Maria Tommasi anasema kwamba, ni utamaduni unaojiondosha kutoka katika uhuru na sheria maadili, kiasi cha kuwageuza wale wote wanaotumbukizwa katika utumwa mamboleo kuwa sawa na bidhaa sokoni. Anaendelea kukiri kwamba, kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na maendeleo kidogo katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo kisheria na kwamba, Jamii imeendelea kuelimishwa juu ya madhara ya utumwa mamboleo unaojipambanua pia kwa ndoa shuruti, biashara haramu ya watoto wanaogeuzwa kuwa ni vijakazi majumbani.

Vatican imeendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kwa njia ya Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi ya kudumu, kupambana na biashara ya utumwa mamboleo. Juhudi hizi zinaungwa mkono na Mashirika ya misaada ya Kanisa pamoja na vyama vya kiraia, vinavyotoa msaada wa hali na mali; sheria na ushauri nasaha pamoja na kuwawezesha waathirika kurudi makwao, tayari kuanza mchakato mpya wa maisha, wakiwa ni watu huru. Uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka anasema Baba Mtakatifu Francisko ni chanzo cha biashara haramu ya binadamu.

Baba Mtakatifu kwa kuguswa na “majanga” haya ya maisha, hivi karibuni aliitisha mkutano wa kikosi kazi kutoka katika Baraza la Kipapa la Taasisi za Sayansi na Sayansi Jamii kwa kushirikiana na Shirikisho la Madaktari Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia kupembua na kubainisha njia sahihi zinazoweza kutumiwa na Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu kisayansi.

Askofu mkuu Silvano Maria Tommasi anabainisha baadhi ya mikakati inayoweza kutumiwa na Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu: kwanza kabisa ni kuanzisha na kuendeleza utamaduni wa usajili wa vizazi na vifo; sheria makini na zinazotekelezeka ili kuzuia biashara haramu ya binadamu. Kuimarisha ulinzi na usalama mipakani pamoja na kuhakikisha kwamba, wahusika wanafikishwa mbele ya mkono wa sheria.

Nchi husika hazina budi kuwa na mikakati na sera makini za ajira hususan miongoni mwa vijana sanjari na kufanya maboresho katika sekta ya elimu na afya; kuimarisha misingi bora ya kifamilia, ili familia ziweze kutekeleza dhamana na wito wake katika Jamii pamoja na kusimamia na kutekeleza haki msingi za binadamu sanjari na utawala bora.

Serikali mbali mbali hazina budi kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ili kuhakikisha kwamba, biashara haramu ya binadamu inakomeshwa kutoka katika uso wa dunia, kwani inadhalilisha utu na heshima ya binadamu.








All the contents on this site are copyrighted ©.