Matumizi ya ndege za "droni" hayana budi kudhibitiwa kimaadili!
Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za
Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, hivi karibuni, alizungumzia kuhusu mwelekeo
wa kimaadili katika matumizi ya ndege zisizokuwa na rubani, kwani zinaweza kusababisha
maafa kwa watu wasiokuwa na hatia pamoja na kuwaletea watu madhara ya kisaikolojia.
Jambo la msingi
kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kulinda na kutetea
haki msingi za binadamu; maisha ya binadamu yakipewa kipaumbele cha kwanza.
Matumizi
ya ndege zisizokuwa na rubani zinazojulikana kama “droni” yameendelea kuongezeka katika
maeneo yenye vita, mgogoro na kinzani za kijamii. Ni teknolijia inayosaidia kupunguza
matumizi ya wanajeshi katika migogoro ya kivita. Kumbe, matumizi ya ndege hizi hata
kama yanaonesha kuwa na faida kubwa, hayana budi kusimamiwa na: sheria, kanuni na
maadili, kwani wakati mwingine madhara yake yamekuwa ni makubwa kwa raia na mali zao.
Hii inatokana na ukweli kwamba, hakuna uwazi wa taarifa na wakati mwingine
teknolojia hii inapania kutoa faida kubwa kwa watengenezaji, badala ya kuzingatia
gharama ya maisha, mali ya raia husika na sanjari na madhara ya kisaikolojia na kiuchumi
kwa kuishi daima katika hali ya wasi wasi. Haya ni mambo ambayo kimsingi yanapaswa
kuangaliwa na Jumuiya ya Kimataifa katika kuhalalisha matumizi ya “droni”.
Kuna
haja ya kuangali pia uwajibikaji wa wale wanaotumia vifaa hivi, kwani wakati mwingine
yamekuwepo makosa ya kibinadamu na madhara yake yakawa ni makubwa kwa maisha ya watu
na mali zao. Hapa kuna haki ya kimataifa, ni nani atakeywajibishwa kwa makosa ya kibinadamu
yanayoweza kutendwa na “droni” katika maeneo ya kivita?
Hapa Askofu mkuu Silvano
Maria Tomasi anasema, kuna haja ya kukazia ukweli, uwazi na uwajibikaji. Matumizi
ya silaha zinazojiendesha zenyewe hayana budi kudhibitiwa sana. Mtu aliyeandaliwa
barabara; wenye habari kamili na makini katika matumizi ya silaha za “droni” ni muhimu
sana, ili kuweza kufikia uamuzi wa kimaadili kwa kuongozwa na busara. Matumizi ya
roboti katika masuala ya vita ni jambo ambalo linapaswa kufanyiwa utafiti mkubwa zaidi
kabla ya Jumuiya ya Kimataifa haijaanza kuhalalisha matumizi yake.
Utafiti
unaonesha kwamba, athari hizi si tu kwa walengwa, bali hata kwa askari wanaozitumia,
ndiyo maana sheria na kanuni maadili hazina budi kuzingatiwa katika vita kwa nyakati
hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kuna hatari kwamba, teknolojia ya matumizi
ya “droni” ikasambaa na hivyo kuhatarisha amani na usalama duniani.