Makanisa ya Kiprotestanti yahamishia Makao yake makuu kutoka Geneva kwenda Hannover!
Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni hivi karibuni
alizindua Makao Makuu Mapya ya Makanisa ya Kiprotestanti huko mjini Hannover, Ujerumani
baada ya Makanisa haya kuhamisha Makao makuu yake kutoka Geneva, Uswiss ambako yalikuwepo
huko kwa miaka 65. Makanisa haya yameenea katika nchi mbali mbali duniani na ni mwanachama
wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni.
Uamuzi wa kuhamisha Makao makuu ulitolewa
hivi karibuni na Kamati tendaji ya Makanisa ya Kiprotestanti baada ya kuona kwamba,
wanaweza kushindwa kumudu gharama za pango na uendeshaji wa shughuli za Makanisa kutokana
na kupanda kwa gharama ya maisha mjini Geneva.
Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa
Ulimwenguni anawatakia kheri na baraka katika Makao Makuu mapya na kwamba waendelee
kushikamana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kwa ajili ya ushuhuda wa
pamoja. Kama wajumbe wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni waendelee kusimama kidete kulinda
na kutafuta haki katika masuala ya kijamii na kiuchumi sanjari na kuunga mkono juhudi
za Makanisa ambayo yako kwenye migogoro na kinzani za kivita kama vile Sudan ya Kusini
na Syria.
Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anawaalika Makanisa
wanachama kuungana pamoja ili kufanya hija ya haki na amani duniani.