Ratiba elekezi ya Ibada zitakazoongozwa na Papa Francisko
Monsinyo Guido Marini, Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa anaonesha kwamba, Baba
Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Mwaka wa
Kanisa, sanjari na Siku ya Mia Moja ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani, tarehe 19 Januari
2014, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu,
Jimbo kuu la Roma.
Tarehe 25
Januari 2014, Siku kuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa mataifa,
Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Masifu ya Jioni yatakayofanyika
kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, nje ya kuta za Roma. Hiki kitakuwa pia ni kilele
cha kufunga Juma la kuombea Umoja wa Wakristo ambao kwa Mwaka huu unaongozwa na kauli
mbiu, Je, Kristo amegawanyika? Ibada hii itaanza saa 11:30 Jioni kwa Saa za Ulaya.
Tarehe
2 Februari 2014, Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni, sanjari na Maadhimisho ya Siku
ya 18 ya Watawa Duniani iliyoanzishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu
anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa na
Kazi za Kitume.
Tarehe 16 Februari 2014, Jumapili ya VI ya Kipindi cha Mwaka
wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu
kwenye Parokia ya Mtume Thoma, Jimbo kuu la Roma.
Tarehe 22 Februari, 2014,
Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko, kuanzia saa 5:00 kwa
saa za Ulaya anatarajiwa kuwasimika Makardinali Wapya 19 walioteuliwa hivi karibuni.
Tarehe
23 Febuari 2014, Baba Mtakatifu ataadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kushirikiana
na Makardinali wote wapya. Kama kawaida, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itaendelea
kukujuza yale yanayojiri katika maisha na utume wa Kanisa hapa Vatican na kutoka sehemu
mbali mbali za dunia.