2014-01-21 07:35:57

Biashara haramu ya binadamu ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu!


Shirikisho la Wakristo dhidi ya biashara haramu ya binadamu, COATNET, linafanya mkutano wake huko mjini Madrid, ili kujadili pamoja na mambo mengine biashara ya binadamu kwa lengo la kupata nguvu kazi; yaani wafanyakazi wa majumbani, tatizo linaloendelea kukua na kuongezeka siku hadi siku. RealAudioMP3

Wajumbe wanapenda kuchukua fursa hii kubainisha mbinu mkakati utakaoweza kutumika katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu kwa siku za usoni.

Shirikisho la COATNET linajumlisha Mashirika 37 ya Kimataifa, mengi ni yale ya Caritas yanayoendelea kuhamasisha ufahamu wa madhara ya biashara haramu ya binadamu na mikakati inayoweza kutumika ili kukomesha biashara hii ambayo ina dhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kuna mamillioni ya watu yanayofanyishwa kazi za suluba kwa ujira kiduchu na huo unakua ni mwanzo wa ukosefu wa haki msingi za kijamii. Ukosefu wa fursa za ajira pamoja na athari nyingine za myumbo wa uchumi kimataifa ni kati ya mambo yanayosababisha watu wengie kusaka fursa za ajira hata kama wananyonywa kiasi gani, kwani wanatumaini kwamba, walau mkono utaweza kwenda kinywani na hivyo kusaidia mchakato wa maboresha ya maisha.

Takwimu za Shirika la Kazi Duniani, ILO zinaonesha kwamba, kuna jumla ya watu zaidi ya millioni 21 duniani kote wanaofanya kazi shuruti. Maeneo yaliyokithiri ni pamoja na: wafanyakazi wa ndani; wafanyakazi katika mashamba makubwa makubwa, sekta ya ujenzi, uzalishaji na Sanaa za Maonesho.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alipokuwa anazungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican amekazia kwamba, biashara haramu ya binadamu ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuunganisha nguvu zake ili kupambana na biashara hii haramu pamoja na kuwasaidia waathirika wa biashara hii. Jumuiya ya Kimataifa, isimame kidete kulinda na kutetea haki jamii; isaidie maboresho ya kiuchumi, ili familia ziweze kumudu gharama za maisha.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Caritas Internationalis linaiwezesha na kuiunga mkono COATNET katika sera na mikakati yake ya kupambana na biashara haramu ya binadamu. Mjini Madrid, wajumbe wanajadili kuhusu sheria za biashara haramu ya binadamu kwa watumishi wa majumbani; vyombo vinavyoweza kutumika kupambana na biashara hii pamoja na kuhakikisha kwamba, wafanyakazi wahamiaji wanapata haki zao msingi.

COATNET ina wanachama wake kutoka Ulaya, Asia, Amerika na Afrika.








All the contents on this site are copyrighted ©.