2014-01-21 11:11:37

Bi Catherine Samba-Panza achaguliwa kuongoza Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati


Wajumbe wa Baraza la Mpito nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati, limemchagua Bi Catherine Samba Panza, mwenye umri wa miaka 56 Meya wa Jiji la Bangui, kuwa Rais wa Kipindi cha Mpito nchini humo. Rais mteule ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mwanamke wa kwanza kuongoza Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati anayo changamoto kubwa ya kuhakikisha kwamba, anahitisha uchaguzi mkuu kabla ya mwisho mwa Mwaka 2014.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema, pengine huu ni mtihani mkubwa kutokana na ukweli kwamba majengo mengi ya Serikali yameharibiwa vibaya kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo iliyozuka Mwezi Machi 2013 baada ya Serikali halali kupinduliwa na Kikosi cha Seleka. Rais mteule amewataka wanajeshi wa Seleka na Balaka kusitisha mapigano na Jumuiya ya Kimataifa kusaidia ujenzi wa nchi utakaojikita katika ukweli, haki, amani na upatanisho wa kitaifa.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon amempongeza Rais Catherine Samba Panza kwa kuchaguliwa kwake na kwamba, huu ni mwanzo wa mchakato wamabadiliko ya kweli nchini humo. Changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata msaada kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa ili kukabiliana na hali ngumu kwa sasa







All the contents on this site are copyrighted ©.