2014-01-20 10:32:59

Wapokot na Waturkana bado wanapambana!


Jumuiya ya Wapokot na Waturkana nchini Kenya bado wanapambana, licha ya taarifa za vyombo vya habari kwamba, Jamii hizi za wakulima na wafugaji zimejipatanisha na hivyo kuanza mchakato wa ujenzi wa haki, amani na upatano. Hayo yamesemwa na Askofu Dominic Kimengich wa Jimbo Katoliki la Lodwar, Kenya katika mahojiano maalum na Shirika la Habari za Afrika, CISA, mwishoni mwa Juma.

Hadi sasa jitihada za Serikali ya Kenya kuzipatanisha Jumuiya hizi mbili bado hazijazaa matunda yanayokusudiwa yaani amani na utulivu kati ya Jamii hizi mbili zinazojihusisha na kilimo pamoja na ufugaji. Wanasiasa wanatoka katika eneo hili bado hawajaanza kujitokeza ili kusuluhisha mgogoro huu unaoendelea kusababisha maafa kwa watu na mali zao.

Viongozi wa Kanisa Katoliki wanaendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa Jadi kutoka katika Jamii za Wapokot na Waturkana, ili kuweza kuleta suluhu ya mgogoro huu kuanzia ngazi ya chini kabisa, ili hatimaye, amani na utulivu viweze kurejea tena katika eneo hili ambali limekuwa ni chanzo cha mapigano ya mara kwa mara kati ya makabila haya mawili.







All the contents on this site are copyrighted ©.